Na Nickson Mkilanya, Morogoro
WATU watatu wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na mvua iliyonyesha katika Kijiji cha Mngazi Tarafa ya Bwakila Juu katika
Wilaya ya Morogoro.
Waliokufa katika tukio hilo ni Richard Abias na Adolf Kunambi (20) ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Milengwelengwe pamoja na Abdalla Kibwe (12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mngazi.
Akizungumza wakati wa mazishi ya watoto hao katika kijiji cha Mngazi, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Mwambungu alisema kuwa tukio hilo limetokea siku Machi 25 mwaka huu saa 10 jioni wakati anafunzi hao wakicheza mpira wa miguu kati ya timu yao na Kitongoji cha Gomelo ya Kijiji cha Kisaki stesheni katika wilaya hiyo.
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa wanafunzi walionusurika katika tukio hilo na kulazwa katika Zahanati ya Mngazi alisema kuwa ,haikuwa mvua kubwa na walidhani kama ingeweza kuleta madhara ya vifo,
Naye Mganga wa Zahanati ya Mngazi Bw. Japheti Ganje alisema kuwa, awali alipokea majeruhi 14 na kwamba wawili amepealekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro baada ya hali zao kuwa mbaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Kibena Kingo alisema licha ya kuhuzunishwa na vifo hivyo, lakini pia ni vigumu kwao kuvidhibiti kwa kuwa vinatokana na janga la kiasili, na kwamba tayari radi ilimejeruhi na kusababisha vifo vya watu wawili mapema mwezi huu katika Kata ya Bwakila chini wilayani hapa na kubomoa nyumba 45.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Issa Machibya na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Bw. Innocent Kalogeres walishiriki katika mazishi hayo kwa nyakati tofauti wazazi wa wa watoto waliofariki katika tukio hilo kutotafuta mchawi kuhusu tukio hilo na kuwataka kuwaamini kuwa hayo ni mapenzi yake Mwenyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment