15 March 2011

'Tiba Liliondo inaimarisha ndoa'

*Walioitumia wafurahia matokeo, wasimulia
*Mgonjwa atoka Afrika Kusini akiwa na drip
*Mzee apotea baada ya kunywa dawa ya babu

Na Gladness Mboma

DAWA inayotolewa na Mchunngaji Mstaafu wa KKKT (Babu), Bw. Ambilikile Mwasapile katika
Kijiji cha Samunge, Loliondo imeelezwa na baadhi ya watu walioitumia kuwa mbali na kutibu magonjwa mengine sugu imeimarisha ndoa zao kwa kuwaongezea nguvu za kiume.

Mmoja wa watu wa watumiaji wa dawa hiyo, amewaambia waandishi wa habari mjini Arusha kwamba ndoa yake ilikuwa inalegalega kutokana na kuugua kisukari kwa muda mrefu na hivyo kutokuwa na uwezo katika tendo hilo la ndoa.

"Huwezi kuamini ndugu waandishi sasa hivi niko fiti, muulize hata mke wangu huyu hapa, atawaeleza sasa hivi tumerudi upya. Ninakula nyama na pia ninakunywa soda. Sichagui na kama hamuamini nendeni mkanywe na kisha mtaona mabadiliko yake," alisema.

Kutokana na kauli hiyo, mke wa shuhuda huyo aliinama chini huku akicheka.

Dawa hiyo ambayo haijathibitishwa kisayansi, imeendelea kuvuta maelefu ya watu kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi, akiwamo mgonjwa mmoja kushushwa katika helkopta ambayo inadaiwa kutoka Afrika Kusini akiwa na dripu kwenye machela, kwa ajili ya kupata tiba hiyo, na baada ya kunywa dawa aliamka mwenyewe.

Mwandishi wa habari hizi aliyefika katika eneo la tukio na makala yake zaidi ukurasa wa 13 wa gazeti hili, alishuhudia mgonjwa huyo akiwa amebebwa kwenye machela akiwa ajitambui.

Baada ya kufikishwa kwa mchungaji Mwasapile na kunyeshwa dawa aliinuka mwenyewe na kisha kuwauliza wenzake yuko wapi na amefika fika vipi, ndipo wenzake walipomueleza kuwa amshukuru babu kwa sababu ndiye aliyemponya.

Mtu huyo ambaye bado ni kijana lakini ugonjwa unaonekana kumzeesha alimwendea babu na kumshukuru na kisha kwenda mwenyewe kwenye helkopta na kupanda bila ya kushikiliwa huku wananchi wakimzonga na kumtaka ashuke.

Watu mbalimbali kutoka nchi jirani ikiwemo Kenya, Uganda na Rwanda wanamiminika kwa wingi huku mabasi yao mengi yakiwa yamekwama njiani kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu.

Mchungaji Mwasapile juzi alisema kwamba kwa wale wenye ugonjwa wa UKIMWI iwapo watakunywa dawa hizo na kisha wakapata tena ugonjwa huo hatopona kwa sababu atakuwa amemkosea Mungu hata kama atakunywa dawa.

Mchungaji huyo alisema kuwa wagonjwa wasioamini dawa hiyo wanaweza kuendelea kunywa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI, lakini yeye anaamini kwamba hata wasipokunywa hizo dawa watapona kutokana na dawa hiyo kutibu ugonjwa huo baada ya siku saba.

Wakati Mchungaji akizungumzia hilo, mwanamke mmoja ambaye alikuwa akimsikiliza alikimbia na kwenda kuwaeleza wanawake wenzake ambao walikuwa kwenye gari kwamba "babu amasema kama ukirudia ngono na kisha ukapata tena UKIMWI huponi, mimi nikirudi simpi mume wangu kwa sababu alikuwa siyo muaminifu bora niachike," alisema.

Bw. Said Athumani yeye alisema kwamba haoni sababu ya watu kuendeleza tena tendo la ngono hovyo wakati amepona na kushauri watu watulie katika ndoa zao kwa sababu dawa hiyo imekuja kama bahati.

Katika kuonyesha kwamba dawa ya Babu ina nguvu kubwa zenye miujiza, watu mbalimbali ambao wanafika wakiwa hawajitambui wameendelea kupona huku wengine wakiwa hawaamini na kuanza kuangusha nyimbo za kufurahia uponyaji.

Mzee apotelea kwa babu

Wakati huo huo, mwandishi Peter Saramba anaripoti kutoka Arusha kuwa Mzee Piniel Kingori (65) aliyekwenda Loliondo kunywa dawa khiyo amepotea na hajulikani alipo zaidi ya siku 10 tangu alipoochana na wenzake.

Akizungumza nyumbani kwake jana, mke wa mzee huyo, Bibi Anna  Kingori alisema mumewe aliondoka na wenzake wanne kwenda Kijiji cha Samunge wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Machi 4, mwaka huu lakini hadi sasa hajarejea nyumbani licha ya wenzake kurudi.

Aliwataja waliondamana na mumewe kwenda kupata tiba ya inayotolewa na mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru, Bw. John Saitabahu, Bw. Bethwel Mbesere, Bw. Saul Mbesere na mke wa Bw. Saitabahu aliyemtaja kama Mama John.

Alisema siku ya tukio mumewe aliyekuwa akisumbiliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu aliamka alfajiri ya Saa 10 tayari kwa safari kama alivyoahidiana na wenzake kwenda Loliondo ambapo kabla ya kutoka alimuomba wasali na baadaye kumuomba amsindikize barabarani baada ya kuwasiliana na wenzake waliomwambia wako njiani kuja kumpitia.

Niliona ajabu kidogo kuniomba nimsindikize kwani siyo kawaida yake. Nilitoka na kumsindikiza hadi mlangoni lakini aligoma kwenda akisisitiza nimsindikize hadi nje, ombi ambalo nililikubali na kumsindikiza hadi tulipokutana na gari iliyowapakia wenzake na baada ya kusalimiana waliondoka nami nikarejea ndani, alisema Mama Anna.

Alisema ilipotimia Saa 10 jioni siku hiyo alijaribu kupiga simu ya mmoja wa watu walioondoka na mumewe ili kujua iwapo wamefika salama na kunywa dawa lakini simu hiyo ilikuwa haipatikani na hata alipojaribu siku iliyofuata Machi 5, mwaka huu pia haikupatikana.

Baada ya kuwasiliana na watu wengine nilielezwa kwamba eneo la kijiji cha Samunge hakuna mawasiliano ya simu hivyo nililazimika kusubiri na ilipofika Jumatatu ya Machi 6, mwaka huu ndipo nilipojaribu tena simu ile na ikapatikana lakini maneno niliyopewa na Mzee Saitabahu ya kuniuliza iwapo mume wangu alifika salama yalinichanganya kwani mimi nilijua wako wote,รข€ alisema Mama Anna.

Alisema baada ya kumweleza mzee Saitabahu kuwa mumewe hajarejea na kumhoji imekuwaje waliondoka wote halafu yeye (Saitabahu) amuulize kama kafika nyumbani, mzee huyo alionyesha mshangao huku akiendelea kuguna hadi simu ilipokatika bila kupata jibu lolote na baadaye mmoja wa waliokwenda na mumewe, Bw. Mbesere alifika nyumbani kwake kupata uhakika kama kweli hajafika.

Kwa mujibu wa Bw. Mbesere aliyekaririwa na Mama Anna, msafara wao ulifika kijiji cha Samunge Saa 7 mchana wa Machi 4, mwaka huu na kukuta foleni kubwa ya kwenda kunywa dawa na hivyo kulazimika kusubiri hadi Machi 5, Saa 4 asubuhi walipofanikiwa kunywa dawa.

Lakini Mzee Bethwel alinieleza kuwa walipofika na kukuta foleni kubwa mwenzao, yaani mume wangu alishuka kwenye gari na kujipenyeza hadi akafanikiwa kunywa dawa mapema kabla ya wenzake na kurejea kwenye gari kuwaaga kuwa yeye anaondoka kwa usafiri mwingine ambao haukujulikana ni wa aina gani.

Hadi hii leo hajaonekana, mimi nimemuachia Mungu ndiye anayejua. Sisi tunaendelea kumuombea awe salama aliko,alisema mama huyo.Tayari ndugu kwa kushirikiana na waliokwenda na mzee Kingori kwa babu kunywa dawa wametoa taarifa polisi na jana kulikuwa na harakati za kutuma kikosi maalumu cha wana ndugu kwenda Loliondo kumtafuta mzee huyo ambaye ni mstaafu wa kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre cha mjini hapa.

Kinachowachanganya zaidi ndugu, jamaa na marafiki ni taarifa kuwa kuna baadhi ya watu wasiojulikana waliokufa njiani njiani wakienda au kurudi kutoka Samunge.

1 comment:

  1. ukiamini,usiamini wewe nenda kwa babu hujui labda ni bahati yako, wacha kuogopa macho ya watu hii ni shida yako, kama hali ya kifedha ya kufika huko ni shida, tafadhali muone mmbunge wako, au peleke kilio chako kwa mzee mengi!!!

    ReplyDelete