Na Tumaini Makene
SPIKA wa Bunge, Bi. Anne Makinda naye pia amesema takwimu za uchumi zinazoonesha kuwa umekua haziwiani na halisi ya maisha Watanzania, wanaozidi kuwa maskini
wakati serikali imeshindwa kuongeza vyanzo vya mapato na kueandelea kuwaumiza watu kwa kufatilia vyanzo vile vile mara kwa mara.
Spika Makinda pia alisema kuwa serikali bado haijatumia maeneo mengine yanayoweza kuwa vyanzo muhimu vya kugharamia bajeti yake, badala yake inajishughulisha zaidi ya vyanzo vichache hali inayosababisha kero kwa wananchi.
Akisema kuwa hali hiyo inaletea uongezekaji wa gharama katika kufanya biashara nchini kwa sababu ya kodi kubwa katika maeneo machache.
Katika hotuba yake iliyosomwa jana Dar es Salaam na Naibu Spika, Job Ndugai, katika ufunguzi wa semina ya wabunge kuhusu usimamizi wa bajeti, Spika Makinda alisema takwimu zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua, lakini maisha ya mwananchi wenye kipato cha chini yamekuwa magumu.
"Hali hii ni changamoto kwetu sisi wabunge kuishauri serikali wakati tukichambua Bajeti ya Serikali kwenye Kamati zetu; maeneo ambayo yakiwezeshwa vizuri yatasaidia kupunguza gharama ya maisha ya Mtanzania wa kawaida," alisema Bw. Ndugai.
Aliongeza kuwa suala la uchambuzi wa bajeti ya serikali ni muhimu hasa katika kuangalia utekelezaji ilivyotekelezwa na Mpango wa Bajeti wa Serikali kwa mwaka 2011/2012.
Alitoa rai kwa wabunge kujadili na kuishauri serikali kuhusu kuweka vipaumbele vichache vinavyotekelezeka ambavyo vitalenga kusaidia makundi ya watu walio wengi na kusaidia kupunguza umaskini.
Pia alizungumzia umuhimu wa ugawaji wa rasilimali ufanyike kwa kuzingatia vigezo na malengo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, yaliyowekwa.
"Katika semina hii Mamlaka ya Mapato Tanzania watatuelezea mifumo ya kodi mbalimbali inayotumika kukusanya mapato na hatimaye serikali ijipangie bajeti yake kutokana na makusanyo hayo. Tutapata fursa ya kuelewa changamoto zinazoikabili mamlaka katika eneo hili la kodi ikiwemo misamaha mikubwa ya kodi.
"Natumaini waheshimiwa wabunge mtatoa michango yenu kwa kina hasa katika maeneo ya vyanzo vipya vya mapato. Ni dhahiri serikali bado haijayashika maeneo mengine ambayo yanaweza kuwa vyanzo muhimu vya kugharamia bajeti yake. Matokeo ya hali hii ni uwezekano wa kujihusisha na vyanzo vichache vya kila siku, mwaka.
"Ambapo hapo baadae zinajengeka kuwa kero kwa wananchi. Hali hii inaletea uongezekaji wa gharama katika kufanya biashara nchini kwa sababu ya kodi kubwa katika maeneo machache. Aidha kuletea ubadhirifu kuletea tatizo la kuepuka kulipa kodi, kukwepa kulipa kodi na hata rushwa," alisema.
Akizungumzia juu ya ukuaji wa uchumi kutosaidia uchumi mdogo ili kuinua maisha ya kila siku ya wananchi walio wengi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Kabwe Zitto alisema kuwa inasababishwa na kutotumika ipasavyo kwa mapato yanayotokana na sekta zinazokua kwa kasi.
"Sekta zinazokua haziwagusi watu moja kwa moja, kwa mfano mawasilinao, madini na nyingine ilitakiwa sasa kuwepo na tafsiri katika uchumi mkubwa kwenda uchumi mdogo katika maisha ya wananchi kwa kutumia mapato ya sekta zinazokua kwa kasi.
"Kwa mfano mapato hayo yatumike kuwekeza katika umeme vijijini, upatikanaji wa maji vijijini, ujenzi wa miundo mbinu mingine vijijijni, maana hizi ndizo kero wanazolalamikia wananchi kila siku...hizi zinaweza kutumika kutengeneza ajira.
"Tatizo ni kwamba hakuna kiongozi anaye-sense kuwa tuko katika matatizo makubwa, nchi haiendi, na dalili ya kuwa hawa-sense ni jinsi ambavyo huoni initiatives (jitihada) zozote za kuondoa au kero za watu...ni wakati mwafaka sasa tujikite katika uzalishaji, tuwaambia watu kuwa ni wakati wa kuzalisha ili tujiletee maendeleo," alisema Bw. Zitto.
No comments:
Post a Comment