LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amewajia juu makocha Kenny Dalglish na Graham Taylor kutokana na hulka yake dhidi ya waamuzi.Ferguson
anakabiliwa na mashtaka mbele ya Chama cha Mpira wa Miguu England (FA), baada ya kumshutumu mwamuzi Martin Atkinson, baada ya Manchester United kufungwa mabao 2-1 na Chelsea.
Kocha wa Liverpool, Dalglish na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England Taylor, walimtaka Ferguson aweke mawazo yake moyoni na si kusema ovyo.
Lakini Ferguson alisema juzi kuwa watu wana kumbukumbu fupi na akasema yeye huamua kutosema lolote, wakati makocha hao wanapowashutumu waamuzi.
Baada ya kushuhudia Chelsea, ikichukua pointi zote tatu katika Uwanja wa Stamford Bridge mwanzoni mwa mwezi huu, Ferguson alisema mechi hiyo ilikuwa ikihitaji mwamuzi atakayechezesha kwa haki na alikuwa akitazamia hali ingekuwa mbaya zaidi mara tu baada ya kugundua mwamuzi atakuwa Atkinson.
Alipohojiwa baada ya mashtaka ya FA, dhidi ya Ferguson ya utovu wa nidhamu kutokana na matamshi yake, Dalglish alisema yeye na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo, wanaheshimu kampeni ya kuheshimu ambayo inawataka makocha kuwaunga mkono waamuzi.
Dalglish akaongeza: "Wakati mwingine unafikiri wale wanaopayuka zaidi ndiyo wananufaika na maamuzi na hiyo kwa kweli si haki."
Shutuma za Taylor dhidi ya Ferguson, zilikuwa ni za moja kwa moja, akitumia gazeti la Daily Express akimwita 'mnafiki' akadai wakati mwingine tabia yake si ya kutarajiwa na 'mtu mwenye haiba kama yake'.
Ferguson, hata hivyo amewashambulia wadau hao wawili wa soka ya England kutokana na shutuma dhidi yake.
No comments:
Post a Comment