Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema kuanzia msimu ujao, Ligi Kuu ya soka Tanzania bara itasimamiwa na Kamati Ndogo ya Ligi hiyo, ili iwe ya
uhuru.
Hatua hiyo imefikiwa katika Mkutano Mkuu wa kawaida wa shirikisho hilo, uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Jumamosi Ukumbi wa Water Front jijini Dar es Salaam ambapo mkutano huo ulitoa pendekezo hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah alisema kamati hiyo itaanza kazi Julai, mwaka huu baada ya Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo kulijadili suala hilo.
"Mkutano umependekeza na litapelekwa kwa Kamati ya Utendaji, ili iipangie kazi na jinsi itakavyoendesha shughuli zake ili isije kuingiliana na Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo," alisema Osiah.
Alisema ana uhakika kamati hiyo itapunguza malalamiko ambayo wamekuwa wakiyapata katika michezo mbalimbali kutokana na kamati hiyo, itakuwa huru kwa kuamua kila jambo pekee bila kushirikisha kamati nyingine.
Katibu huyo alisema ligi mbalimbali duniani, zinaendeshwa kwa mtindo huo ila wao watakachofanya ni kuangalia ligi hizo zina upungufu gani kwa kutumia mfumo huo, ili na wao wasije kuingia katika migogoro ambayo imezitokea nchi zingine zinazoendesha ligi kwa mfumo huo.
Wakati huo huo, Osiah alisema TFF imekubali kuilipa Kagera Sugar gharama walizopata kwa kuahirisha mara mbili mchezo wa dhidi ya Simba, ambao sasa utapigwa leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Alisema walipokea malalamiko kutoka kwa uongozi wa Kagera Sugar ukidai unatumia gharama kubwa kukaa jijini Dar es Salaam kusubiri mchezo wao dhidi ya Simba.
"Tuliyapokea malalamiko yao na katika kuyaangalia tukagundua wana hoja, kwani walidai fedha zilizotolewa na wadhamini kukaa jijini hazitoshi, hivyo kwa kuliona hilo TFF imeamua kuwalipia gharama zao kwa siku zilizoongezeka," alisema Osiah.
Alisema licha ya Kagera kulalamikia sana suala la kuahirisha mchezo huo, lakini kikanuni inaruhusiwa na ndiyo maana TFF imeliona hilo na kulifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment