15 March 2011

Tathimini ya maafa Gongolamboto yakamilika

Na Peter Mwenda

KAMATI ya Maafa iliyokuwa ikihakiki nyumba zilizobomoka kwa mabomu yaliyolipuka kambi ya Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya
Gongolamboto imemaliza kazi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Leonidas Gama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala alisema wakati wa uhakiki huo walikabiliana na changamoto mbalimbali zilizochelewesha kukamilika kwa haraka ikiwemo wananchi kutoa taarifa za uongo.

Alisema nyumba zilizopitiwa na kuhakikiwa ni 3,000 na taarifa yake itapitiwa na Kamati ya Maafa ya Mkoa kabla ya kutoa taarifa ya nyumba ambazo zitajengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na zile zitakazokarabatiwa.

Bw. Edgar Senga ambaye ni Ofisa Maafa Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu aliyeongoza timu hiyo alisema walipata wakati mgumu kufikia waathirika kutokana na barabara kutofikika kwa urahisi na wengine kukarabati nyumba zao kabla ya kuhakikiwa.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Urusi kwa mara nyingine imetoa misaada ya mahema, chakula na nyama ya kwenye makopo vyote vikiwa na uzito wa tani 35.

Akikabidhi msaada huo, Balozi wa Urusi nchini, Bw. Alexander Rannikh alisema serikali yake ambayo awali ilitoa dola 100,000 za Marekani inaungana na Watanzania kuwafariji familia zilizopata maafa ya mabomu ya Gongolamboto.

Wengine waliotoa misaada yao ni Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kinondoni iliyotoa vyakula, fedha na nguo zenye thamani ya sh. milioni 1.4, Mkoa wa Dodoma umetoa hundi ya sh. milioni 27 na mlemavu Bi. Mwintumu Zayumba alitoa nguo, Shirika la Ndege la Kenya lilitoa misaada ya sh. milioni 6.

Akipokea misaada hiyo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Sadiki alisema bado waathirika wa mabomu ya wanahitaji misaada mpaka serikali itakapowajengea nyumba zao na kuwakabidhi wenyewe.

Alisema wananchi, taasisi za umma na mashirika wanaombwa kuendelea kutoa misaada ya kwa waathirika hao ambao bado wanahitaji kula, kuvaa na kusoma.

No comments:

Post a Comment