Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager, imezindua mashindano ya Kombe la Taifa (Kili Taifa Cup) yatakayoanza
kutimua vumbi Mei 7, mwaka huu katika vituo sita nchini.
Mbali na hilo, kampuni hiyo imetenga sh. milioni 800 kwa ajili ya kuendeshea mashindano hayo ambayo bingwa atalamba sh. milioni 40, wa pili sh. milioni 20 na wa tatu sh. milioni 10.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuzindua mashindano hayo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema mashindano ya mwaka huu yameboreshwa kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka iliyopita.
"Tumezindua rasmi mashindano ya Kili Taifa Cup 2011 na kwamba kwetu sisi mashindano hayo yataanza Mei Mosi ambapo tutaanza kufanya promosheni za kwenye magari na za viwanjani, hivyo tunaomba wadau wa soka wakae mkao wa kula," alisema Kavishe.
Alisema lengo lao ni kufikisha soka la Tanzania katika kilele cha mafanikio, kwani wanajisikia fahari kuona vijana ambao hawakuweza kuonekana na timu za Ligi Kuu lakini kupitia mashindano hayo wanaonekana.
Akizungumzia suala la zawadi, alisema zimeongezeka tofauti na mwaka jana ambapo bingwa alipata sh. milioni 35, lakini sasa ni milioni 40 ambapo pia mfungaji bora atajinyakulia sh. milioni 2.5.
Mbali na mfungaji bora, kipa bora, kocha bora, mwamuzi bora na mchezaji mwenye nidhamu kila mmoja atajinyakulia sh. milioni 2 na kwamba kila mechi atachaguliwa mchezaji bora wa mechi ambaye ataondoka na sh. 100,000.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema anaishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kudhamini mashindano hayo kwa mara ya nne mfululizo na kwamba zawadi wanazotoa zitaongeza ushindani katika mashindano hayo.
Aliwataka viongozi wa mikoa kuhakikisha wanatafuta wadhamini wa ziada kusaidia mahitaji yao, kwani TBL haitaweza kushughulikia mambo yote yanayohitajika katika timu na kwamba mwezi ujao mashindano yataanza katika wilaya na baadaye kupata timu ya mkoa.
Akizungumzia suala la vituo, alisema vikuwepo sita ambapo kila kimoja kitakuwa na timu nne na watavitangaza baadaye huku taratibu zingine za kimashindano zipo kama zilivyokuwa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment