14 March 2011

Tamimu amwadhibu Ashraf kwa KO

Na Amina Athumani

BINGWA wa ngumi wa Afrika Mashariki na Kati, Awadh Tamimu, amefanikiwa kutetea ubingwa wake wa ECAPBF kwa kumtwanga kwa KO, raundi ya
sita, Ashraf Suleiman.

Pambano hilo lilifanyika katika ukumbi wa DDC Mliman Park Mwenge na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC)

Akizungumzia matokeo hayo, Ofisa Uhusiano wa TPBC,  Boniface Wambura, alisema Tamimu alitangazwa mshindi na mwamuzi Names Kavishe, baada ya Ashraf kushindwa kuendelea na pambano katika raundi ya saba,  hivyo Tamim kutangazwa mshindi.
 
Pambano hilo lilikuwa la raundi 10 na mabondia hao walikuwa wakipigana uzito wa juu wa kg 105, ambapo kila mmoja aliweza kuonesha uzito wa makonde yake kwa mwenzake.

Katika raundi ya kwanza hadi ya tatu, Ashraf alimwangusha chini Tamimu mara mbili kutokana na makonde mazito aliyokuwa akiyarusha.

Hata hivyo, makonde hayo hayakuweza kumlevya Tamimu kiasi cha kushindwa kuendelea,  katika raundi ya kwanza Tamimu alidondoshwa, na mwamuzi Kavishe alimhesabia, lakini  alisimama na kuendelea na mchezo.

Raundi ya nne hadi raundi ya sita, Tamimu alijitutumua kwa kurejesha mashambulizi kwa Ashraf , ambapo raundi ya saba bondia huyo hakutaka kuendelea na mchezo na kumwezesha Tamim kuendelea kuushikilia ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

Pambano hilo ni la pili kwa mabondia hao kucheza, katika pambano la kwanza, Tamimu alimpiga Ashrafu kwa pointi na Ashrafu kupinga matokeo akiomba mechi ya marudiano.

Ushindi wa Tamimu ulizua tafrani kubwa baada ya bondia huyo kusherehekea ushindi huo kupita kiasi, hali iliyowafanya mashabiki kufikiria kuwa, labda kachanganyikiwa, baada ya muda mfupi, bondia huyo aliondolewa kwa ajili ya kwenda kupumzika.

Katika mapambano ya utanguliz, Seleman Saidi alimtwanga kwa KO, Chilambo Hemed, raundi ya kwanza pambano lililokuwa la raundi nane.

Alphonce Mchumiatumbo akimpiga Ramadhan Kido kwa pointi.

Katika mapambano mengine, Cosmas Cheka alimtwanga kwa pointi Rajab Maoja, Alan Kamote alimshinda  kwa pointi Shadrack Ignus na Manti Abuu alimchakaza kwa KO raundi ya tatu Salum Malemba katika pambano lililokuwa na raundi nne.

Naye, Ofisa Uhusiano wa Aurora Security, ambao ndio wadhamni wa mapambano hayo, Shomari Kimbau, alisema watanzania wanapaswa kujua kuwa, mpaka sasa ni mabondia wawili  wanaopigana katika uzito wa juu na wanafanya vizuri zaidi katika medani ya ngumi za kulipwa.

Alisema kutokana na kiwango kikubwa kilichooneshwa na mabondia hao, Kampuni hiyo ya Aurora imeahidi kuwadhamini mabondia hao katika kuwatafutia mapambano.

Tamim atatafutiwa pambano la ubingwa wa Afrika huku Ashraf akitafutiwa pambano la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment