17 March 2011

Simba yataja 20 watakaoivaa Mazembe

Na Zahoro Mlanzi

KIKOSI cha wachezaji 20 na viongozi watano cha timu ya Simba, kinatarajia kuondoka nchini Jumamosi kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kuumana na
TP Mazembe ya nchini humo Jumapili katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Katika kikosi hicho wachezaji Kelvin Charles, Faraji Kabali na Abdulhalim Humuod wameachwa huku Hilaly Echessa, Joseph Owino na Uhuru Selemani wakibaki kuuguza majeraha yao ya muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili imezipata Dar es Salaam jana, zilieleza kwamba msafara huo utaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' na viongozi wengine wanne ambao wataondoka Jumamosi mchana.

Mbali na viongozi hao, pia kutakuwepo na viongozi wa benchi la ufundi litakaloongozwa na Kocha Mkuu, Patrick Phiri, msaidizi wake, Amri Saidi, Meneja, Innocent Njovu pamoja na daktari ya timu.

"Humuod bado hali yake si nzuri, hivyo benchi la ufundi limeamua aendelee kubaki nchini kuendelea kupata matibabu ila kipa, Kabali na Kelvin Charles wameachwa kutokana na idadi inayotakiwa kwenda kuwa ndogo.

Taarifa hizo ziliwataja wachezaji watakaoondoka ni makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha 'Barthez', mabeki Haruna Shamte, Salum Kanoni, Juma Jabu, Amir Maftah, Meshack Abel, Kelvin Yondani na Juma Nyosso, viungo ni Amr Kiemba, Mohamed Banka na Nicco Nyagawa.

Viungo wengine ni Jerry Santo, Rashid Gumbo, Patrick Ochan, washambuliaji ni Mussa Hassan 'Mgosi', Ally Ahmed 'Shiboli', Shija Mkina, Mbwana Samatta na Emmanuel Okwi.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Clifold Ndimbo kuzungumzia suala hilo la safari alisema maandalizi yanakwenda vizuri na kwamba leo wataanika silaha zao zitakazoivaa TP Mazembe.

Alisema timu hiyo itarejea jijini Dar es Salaam leo na kesho au keshokutwa safari ya kwenda DRC, itaanza ambapo watakwenda kwa ndege ya kukodi.

2 comments:

  1. Timu yetu na wawakilishi wetu tunawatakia safari njema na pia mchezo mwema na mfanikio tele. Tunawaombea Dua! Tuleteeni ushindi! Japo TP mazembe ni wazuri sana, jitahidi mambo yanawezekana kabisaa!

    ReplyDelete
  2. NI VIZURI kujipa moyo, lakini maandalizi yanatia MOYO? TAFAKARI!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete