17 March 2011

Mabondia kibao watemwa timu ya taifa

Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limewatema mabondi kibao katika kikosi cha timu ya taifa ya ngumi iliyotangazwa jana.BFT pia inatarajia
kumwita katika kikosi hicho, bondia Emilian Patrick aliyewahi kukamatwa nchini Mauritius kwa kashfa ya dawa za kulevya.

Akitangaza kikosi hicho Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema wameamua kuita chipukizi wengi katika timu hiyo na kuondoa wakongwe ili kuimarisha zaidi mchezo huo na kwamba wamezingatia umri, uwezo na nidhamu.

"Wapo mabondia wengi mno ambao walikuwepo kwenye kikosi cha timu ya taifa tumewaacha na hii si kama hawana uwezo, bali tumeangalia vigezo mbalimbali ambavyo mchezaji wa taifa anatakiwa kuwa navyo, hususan suala la umri na nidhamu," alisema Mashaga.

Katika kikosi hicho mabondia 28 wamechaguliwa kuunda timu hiyo ya taifa ambao 24 kati yao ni chipkizi, wakati wakongwe waliobakizwa kwenye kikosi hicho ni Selemani na Godfrey James, Kidunda kg. 75 na Boniface Mlingwa kg. 52 (Ngome) na Maximilian Patrick super weight (Magereza).

Mabondia wengine ni John Christian kg. 49 (Kinondoni), Yahaya Maliki (Polisi), Dogo Mussa (Ilala) na Abdallah Kassim (Ngome), ambapo uzito wa kg. 52 ni Nassor Ally (Pwani), Aidan Issa (Rufiji) na  Godfrey Timoth (Morogoro).

Uzito wa kg. 56 ni Ismail Isack (Pwani), Omari Mrisho (Ngome) na Wambura Amiri (Temeke), kg. 60 ni Bosco Bakari (Mwanza), Elias Nkome (Rukwa) na Idd Pialali (Kinondoni), kg. 64 ni Victor Njaiti (Magereza) na Mseven Gosper (Polisi), kg. 69 ni Mohamed Chimbulimbuli (Polisi) na Method Chonga (Pwani).

Pia wamo Abdallah Rashid kg. 75 (Kinondoni) na Juma Ally (Tabora), kg. 81 Abdallah Shaban (Kinondoni), Juma Farahani (Tabora) na Issa Kimanga (Ruvuma) na uzito wa kg. 91 ni Shaban Yusuf (Temeke) na Amos Godwin (Magereza).

Wakati huo huo, BFT imemfungia bondia Renatus Mpandangazi, kutokana na utovu wa nidhamu aliyoufanya katika mashindano ya Klabu Bingwa baada ya kumtukana mwamuzi pamoja na kuvua glove pamoja na head gear na kuvitupa ulingoni, kabla ya pambano kumalizika kati yake na Leonard Machichi.

No comments:

Post a Comment