17 March 2011

Serikali imefika kikomo cha kufikiri-Mbatia

Na Grace Michael

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia amesema kutokana na kufika kikomo cha kufikiri kwa serikali iliyoko madarakani kumeifanya
kushindwa kushughulikia matatizo ya msingi yanayowakabili wananchi.

Kutokana na hali hiyo amewataka wananchi kutoishia kujadili suala la tiba ya Loliondo peke yake badala yake waendelee kujadili na kuibana serikali katika masuala yote nyeti ambayo yalikuwa yameitikisa nchi hivi karibuni.

Masuala hayo aliyataja kuwa ni suala la Dowans, Katiba, mabomu yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi Gongolamboto, suala la umeme, mfumko wa bei, elimu na mengine.

Bw. Mbatia aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu yaliyojiri katika ziara iliyofanywa na chama hicho mkoani Kigoma kwa lengo la kushukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuchagua wabunge wanne wa NCCR-Mageuzi.

Unajua Taifa limechoka kufikiri na ndio maana linabaki lijikita kwenye mambo mengine na kuacha mambo ya msingi. Na utaona hata bunge lijalo nalo litabaki likizungumzia masuala ya kikombe cha babu Loliondo na kama mnakumbuka bunge letu liliwahi kutumia muda mwingi kujadili ushirikina, hivyo pamoja na kuwepo kwa babu Loliondo lakini tusisahau mambo ya msingi, alisema Bw. Mbatia na kuongeza kuwa.

Serikali kwa sasa inafuraha tu kwa kuwa imepumzishwa na mambo mengi kama ya Dowans, katiba na mengine hivyo tusipokuwa macho hata hilo suala la katiba itafika mahali tutaambiwa muda ulikosekana kwa kuwa kila mmoja alikuwa akishughulikia Loliondo, alisema.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Mbatia alisisitiza wananchi kutohama kwenye agenda za muhimu ambazo zinataka kufunikwa na mambo mengine.

Akizungumzia yaliyojiri ziarani Kigoma, Bw. Mbatia alieleza namna alivyosikitishwa na ubovu wa daraja la mto Malagalasi ambalo alisema kuwa linaweza kusababisha maafa muda wowote.

Alisema kuwa daraja hilo likiharibika Mkoa wa Kigoma utatengwa kwa barabara, reli pamoja na anga hivyo kusababisha kero kubwa kwa wananchi wa mkoa huo wakati wanapohitaji kusafiri.

Mwananchi wa Kigoma kwa sasa akitaka kutumia usafiri wa ndege ni zaidi ya sh. 900,000 ili afike Dar es Salaam tofauti na mtu anayetoka Dar es Salaam kwenda India gharama yake ni ndogo, hivyo utaona ni jinsi gani serikali ya Chama Cha Mapinduzi ilivyoshindwa kuongoza na ambavyo haina mwelekeo, alisema.

Alisema kuwa jitihada za haraka zinatakiwa katika kuwakomboa wananchi wa Kigoma kwa kuwa njia zote za usafiri wanazotumia hazina uhakika kutokana na ubovu wa miundombinu iliyopo.

Alieleza kuwa daraja la reli katika mto Malagalasi nalo liko katika hali ya hatari na linaweza kusababisha maafa muda wowote lakini mbali na daraja miundombinu ya reli hiyo ni ya wasi wasi kwa kuwa yapo maeneo ambayo mataluma ya reli yamefunguliwa.

Mbali na hilo, alivitaka vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo na si kutanguliza chuki binafsi katika uandishi wa habari hizo.

Bw. Mbatia alisema baadhi ya habari zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari wakati wa ziara yake mkoani Kigoma zilimhusisha na kukishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitu ambacho alisema hana mpango wa kufanya.

Mimi si msemaji wa CHADEMA...nimehusishwa na mambo mengi imefika hata wakati tunaitwa CCM  lakini niseme tu kwamba nipo kwa ajili ya chama changu kama tulivyosajiliwa, na mambo ya kutuita CCM ni kutaka kutuvuruga tu na kuipa nguvu CCM ambayo imeshindwa hata kuongoza, alisema Bw. Mbatia.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa endapo kuna mwandishi anakichukia chama hicho au Bw. Mbatia atumie njia nyingine ya kumshambulia na si kupotosha habari zilizoandikwa kwa ajili ya wananchi.

No comments:

Post a Comment