21 March 2011

Simba yashindwa kuizuia TP Mazembe

*Yalala 3-1 Stade de la Kenya

Na Mwandishi Wetu, Lubumbashi

MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba jana imeanza vibaya katika mechi yake ya kwanza ya
Klabu Bingwa Afrika, dhidi ya TP Mazembe baada ya kukubali kufungwa mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Stade de la  Kenya mjini hapa.

Mechi hiyo ambayo ilihudhuriwa na mashabiki wengi waliokuwa wakishangilia kwa nguvu, ilianza kwa Simba kulifikia lango la wapinzani wao mapema lakini hata hivyo washambuliaji wake Mbwana Samatta na Mussa Hassan 'Mgosi' hawakuweza kuleta madhara.

TP Mazembe ilipata bao la kwanza dakika ya 11 kupitia kwa Deo Kanda ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa Simba waliozubaa na kupiga shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Kabla ya kufungwa bao hilo, mabeki wa Simba walifanya faulo ambayo wachezaji Kanda na Alain Kaluyitika wa TP Mazembe walipasiana mbele ya mabeki hao walikuwa wajipanga na kusubiri filimbi ya mwamuzi lakini mfungaji baada ya kupasiwa aliachia kombora kali la kushtukiza lililopenya wavuni.

TP Mazembe walifunga bao la pili dakika ya 24 kupitia kwa Narlise Ekanga ambaye aliachia shuti kali la karibu lililomshinda kipa Kaseja ambaye aliruka bila mafanikio.

Simba kipindi cha kwanza walionekana kulinda zaidi goli na kumuacha kipa wa TP Mazembe, Kidiaba kwenda likizo kwa muda mrefu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na TP Mazembe waliongeza bao la tatu dakika 64 kupitia kwa Kaluyitika baada ya kuwalamba chenga mabeki na kuwafanya mabingwa hao kutoka kifua mbele katika uwanja huo wa Stade de la Kenya.

Hata hivyo kabla ya Simba kufungwa bao hilo dakika ya 64, Mussa Hassan Mgosi aliinyima timu bao baada ya kupata nafasi nzuri akiwa na kipa, lakini kutokana na kutokuwa makini alipiga shuti fyongo lililopanguliwa na kipa Kidiaba.

Simba baada ya kufungwa bao hilo ilibadilika na kuanza kutafuta mabao na kupeleka mashambulizi langoni mwa wapinzani ambapo, juhudi zao zilizaa bao dakika ya 76 kwa njia ya penalti iliyotumbukizwa kimiani na Emmanuel Okwi.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi, Younis Yassek wa Misri baada ya kipa wa TP Mazembe Kadiaba kumuangusha OKwi katika eneo la hatari wakati akienda kufunga.

Timu hizo sasa zitarudiana wikimbi zijazo katika mechi itakayopigwa jijini Dar es Salaam, ambayo Simba watalazimika kushinda mabao 2-0 ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika.

4 comments:

  1. Safari imefika MWISHO!!

    ReplyDelete
  2. ushauri wa bure simba waende loliondo kuweka kambi kwa ajili ya mechi ya marudiano hiyo tarehe 2/4/2011 angalau wapunguze idadi ya mabao ktk uwanja wa taifa?

    ReplyDelete
  3. Nyie si wazalendo hata chembe, bali ni wanazi wa YANGA ambayo ingekuwa ndo imecheza jana, ingefungwa si chini ya magoli 10! SIMBA itashinda Dar! Inshalah!!!

    ReplyDelete
  4. hizo ni ndota ya abuniwasi eti Simba iatifunga TP mazembe,nyie wanasimba amkeni!

    ReplyDelete