21 March 2011

CHANETA yahofia kukosa misaada ya IFNA

Na Amina Athumani

CHAMA Cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimesema kinahatihati ya kukosa misaada kutoka Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA) ikiwa ni pamoja na
kufutiwa uanachama wake, baada ya kugundua kuwa Tanzania inapinga kuanzishwa kwa Shirikisho jipya la Netiboli Afrika lililoanzishwa mwaka jana.

Akizungumza Da es Salaam mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Bayi alisema kumekuwa na dalili za Tanzania kukosa misaada ya hali na mali kutoka IFNA, baada ya kubaini kuwa Tanzania inapinga kuanzishwa kwa shirikisho hilo la Afrika, jambo ambalo si kweli.

Alisema kutokana na ukweli kwamba vyama vya netiboli Afrika vya nchi 14 kati ya 18, ambavyo ni wanachama wa IFNA ziliamua kuanzisha  shirikisho jipya la netiboli la Afrika, baada ya kuona Shirikisho la Netiboli la Afrika (CANA) kushindwa kuleta maendeleo yaliyotarajiwa na wanachama wake.

Alisema IFNA inatambua shirikisho jipya ndiyo mwakilishi rasmi wa netiboli katika Afrika na kwamba Tanzania na Uganda ni miongoni mwa nchi 14, ambazo ni waanzilishi wa shirikisho hilo.

"Si kweli kuwa Tanzania inapinga kuanzishwa kwa shirikisho hilo kama IFNA, inavyodai kwani kumekuwa na njama za  viongozi wa CANA kupotosha ukweli juu ya uwamuzi wa wanachama wake kujitoa na kuanzisha shirikisho jipya," alisema.

Alisema hadi sasa Tanzania bado haijajua kama itashiriki michuano ya Mataifa ya Afrika itakayofanyika Msumbiji mwaka huu, kwa kuwa bado mgogoro huo haujamalizika ambapo wameitaka Serikali kufuatilia suala hilo, ili CHANETA na Tanzania kwa ujumla kujua hatma ya CANA na Netibol Afrika.

No comments:

Post a Comment