*Leo ni zamu ya Yanga, Azam FC
Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba jana walicheleweshwa katika safari yao ya kuukaribia ubingwa baada ya kulazimishwa suluhu na
Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Simba sasa inaongoza ikiwa na pointi 45 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 40, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Azam FC yenye pointi 37.
Leo ni zamu ya Yanga na Azam ambazo zinakutana katika Uwanja wa Uhuru katika mfululizo wa ligi hiyo, ambapo katika mchezo huo kila timu itakuwa ikisaka ushindi kwa udi na uvumba ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi.
Mechi ya jana ilianza kwa Kagera Sugar kuliandama lango la Simba lakini hata hivyo kutokana na uchezaji wao wa kucheza pasi nyingi uliwafanya washindwe kutumbukiza mpira kimiani na hivyo kuwapa Simba mwanya kulisakama lango la timu hiyo ambapo dakika ya kumi Mussa Hassan 'Mgosi' alikosa bao baada ya kuunganisha krosi iliyochongwa na Emmanuel Okwi.
Baada ya shambulizi hilo Kagera Sugar ilizinduka na kufanya kuliandama lango la Simba ambapo dakika ya 25, Gaudence Mwaikimba aliyepokea pasi ya George Kavila aliachia shuti kali lililotoka nje kidogo ya lango.
Kipindi cha pili Simba iliingia kwa nguvu na dakika ya 46, Shija Mkina aliyeingia badala ya Mohamed Banka aliachia shuti kali lililookolewa na beki Tonny Ndolo katikati ya mstari baada ya kupishana na krosi iliyochongwa na Juma Jabu.
Themi Felix wa Kagera Sugar dakika ya 56, alishindwa kuipatia timu yake bao baada ya kubaki na kipa Juma Kaseja lakini kutokana na kutokuwa makini akapaisha mpira juu ya mwamba wa goli.
Dakika ya 81, Gaudence Mwaikimba alikosa penalti baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Juma Kaseja. Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi, Paul Mujaya wa Mwanza baada ya Haruna Shamte kumwangusha Paul Ngalyoma aliyeingia badala ya Sunday Hinju.
Kipa Kalwesubula Hannington wa Kagera alitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kuchelewesha muda, awali kipa huyo alikuwa tayari amepewa kadi ya njano.
Baada ya kipa kutolewa nje, Kocha wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja alilazimika kumtoa Felix na nafasi yake kuchukuliwa na kipa mwingine Msafiri Davo, ambaye naye aliumia dakika chache baada ya kuingia na hivyo mpira kusimama kwa dakika tano.
TAFADHALI MSIANDIKE HABARI KIUSHABIKI,..MAANA KICHWA CHA HABARI HIKI.."SIMBA YACHELEWESHWA KUNYAKUA UBINGWA"..kinaonesha mwandishi ni shabiki wa simba.
ReplyDeletesasa wewe ulitaka mwandishi aandike kitu gani?! na wakati huo ndio uhalisia. Anyway inabidi uwe na gazeti lako uandike unavyotaka wewe.
ReplyDeleteNi kweli kabisa mtoa maoni wa kwanza inaelekea hajasoma habari yote iliyoandikwa gazetini na kuifahamu sawasawa.Yeye ndie anaeongelea hiyo habari kwa ushabiki.
ReplyDelete