Na Kulwa Mzee
MWALIMU Revocatus Onesmo (34) wa shule moja ya msingi wilayani Kinondoni anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kughushi matumizi ya kadi ya Bima ya Afya
kwa kumpa mtu mwingine asiye tegemezi kuitumia.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya Afya Kanda Maalumu ya Mashariki, Bw. Raphael Mwamoto alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema Machi 3, mwaka huu mwalimu huyo alifika Hospitali ya Tumaini na kujiandikisha kana kwamba ni mgonjwa, akasaini lakini uchunguzi ulipofanywa kwa kulinganisha kadi zinazorudi na wagonjwa waliolazwa, ikabainika aliyelazwa kwa kutumia kadi hiyo ni Bw. Bakari Magimba (67).
Bw. Mwamoto alisema mzee huyo hayumo miongoni mwa wanaomtegemea mwalimu huyo, hivyo wadau wanapaswa kujua kwamba hujuma hizo zinatambulika na hatua zinachukuliwa.
"Tumeamua kutolipa gharama za mgonjwa huyo ambazo ni zaidi ya sh. milioni 2.5 ili iwe fundisho, na mfuko umelifikisha suala hilo mbele ya sheria, wakati ukifika atafikishwa mahakamani," alisema.
Mkurugenzi alitoa mwito kwa watoa huduma kuhakikisha wanatambua wanachama wanaofika kutaka huduma, kufananisha kitambulisho na mgonjwa anayetaka huduma.
Alisema matukio kama hayo yapo na katika robo mwaka kwa kanda hiyo yameshatokea matatu na yanatokea kwa magonjwa makubwa.
Bw. Mwamoto alisema wamejipanga kukabiliana na hali hiyo na hawatasita kuwachukulia hatua watakaobainika, wamewataka wanachama wasitumie kadi zao kwa watu ambao si tegemezi.
No comments:
Post a Comment