18 March 2011

Serikali yavitolea uvivu vyama vya michezo

Na Amina Athumani

SERIKALI imevitaka vyama vya michezo nchini kutengeneza utaratibu wa kuaminiwa na wadhanini kwa kuwa baadhi ya viongozi wanatumia udhamini
wanaoupata kwa maslahi binafsi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kikao cha pamoja na Chama cha riadha Tanzania (RT) kilichokuwa kinajadili matatizo mbalimbali na mapendekezo ya chama hicho kwa Serikali, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Emmanuel Nchimbi alisema wadhamini wamekua wakigoma kutoa udhamini katika michezo kutokana na kutowaamini viongozi kwakuwa wengi wanamatatizo na maslahi binafsi.

"Unakuta kiongozi anaomba udhamini kwa ajili ya kuiweka timu kambini wakati huo huo anasema watoto wake hajawalipia ada hivi kweli huyo mdhamini ataweza kutoa fedha zake,"alihoji Waziri Nchimbi.

Alisema viongozi wanatakiwa kwanza kujenga utaratibu mzuri wa kuaminika kwa kuwa hakuna mdhamini atakayetaka kutoa fedha zake bila kufikia malengo aliyoyatarajia.

Waziri Nchimbi amevitaka pia vyama vyenye migogoro ya siku nyingi kumaliza migogoro hiyo hususan kwa viongozi ambao wanang'ang'ania uongozi kwa muda mrefu bila ya kuwa na uongozi unaowafikisha kwenye tija.

Alisema ameahidi pia kutoa ushirikiano kwa vyama  vya michezo ikiwa ni pamoja na kuongeza maofisa wa michezo na utamaduni ambapo pia atawawekea utaratibu mzuri  wenyeviti wa mikoa wa kuweza kufikisha mawazo yao kwake ya namna ya kuibua vipaji.

Kwa upande wa RT ambao walitoa malalamiko mengi juu ya Serikali kushindwa kutoa mchango katika kuandaa timu za Taifa, wameitaka serikali kuboresha viwanja vya michezo katika sehemu ya kukimbilia, ikiwa ni pamoja na kusaidia na kuwapa motisha wachezaji ambao watakuwa kambini wakilitumikia Taifa.

No comments:

Post a Comment