18 March 2011

Mosha ang'aka kujadiliwa Yanga

*Ataka wanachama kuheshimu uamuzi wake

Na Elizabeth Mayemba

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga ambaye hivi karibuni alijiuzulu wadhifa huo, amewaomba wanachama na viongozi wa klabu hiyo
kuheshimu maamuzi yake aliyoyachukua na kuacha kuendelea kumfuatilia na kumjadili katika vikao vyao.

Hivi karibuni Mosha aliuandikia barua uongozi wa klabu hiyo, pamoja na wajumbe wote kuelezea nia yake ya kuachia wadhifa huo, kwa madai ya kudhalilishwa na baadhi ya wanachama katika vyombo vya habari, ikiwemo kumtishiwa maisha.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mosha alisema anashangaa kuona watu wakiendelea kumjadili  wakati tayari ameshaondoka kwenye uongozi, badala ya kujadili maendeleo ya klabu.

"Mimi naomba watu waheshimu maamuzi yangu, nimejiuzulu kwa hiari yangu bila kushawishiwa na mtu, hivyo watu wanapokuwa wanakaa vikao vyao naomba nisiwemo kwenye ajenda yoyote," alisema Mosha.

Alisema hivi sasa timu hiyo inakabiliwa na mechi tatu za lala salama ambazo ni muhimu kwao kushinda, hivyo ingekuwa vizuri muda ambao unatumika kumjadili yeye wangeutumia katika kupanga mikakati ya timu hiyo kufanya vizuri mechi hizo zilizosalia.

Mosha alisema ataendelea kuwa mwanachama wa Yanga kama zamani, na wala hafikirii kurudi tena madarakani kwa sasa, kwa kuwa hapo alipoiacha panatosha.

Katika hatua nyingine, kikao cha matawi ya Yanga Mkoa wa Dar es Salaam, kilichofanyika juzi kilivunjika baada ya kuingizwa ajenda ya kumjadili Mosha.

Kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu wa klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani kilikuwa na ajenda mbili, kuzungumzia ushiriki wa timu katika Ligi Kuu Tanzania Bara na nyingine ya kuijadili barau ya kujiuzulu kwa Mosha.

Ilipofika ya kuijadili barua ya Mosha kundi moja la wanachama liliwasilisha barua yao katika kikao hicho na kutaka wasijadili suala hilo kwa madai ni ukiukwaji wa katiba.

Baada ya baada ya kuingizwa hoja hiyo kulitokea mvutano mkali kati ya makundi hayo, kundi la pili lilimtaka Mwenyekiti wa Matawi Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Msumi atoke nje ili wamjadili kwa kitendo chake cha kuwasilisha ajenda hiyo, lakini kundi lingine lilimtaka Mwenyekiti huyo asitoke.

Kutokana na vurugu hizo ndipo kikao hicho kilipovunjika na ajenda hiyo ya pili haikujadiliwa tena.

No comments:

Post a Comment