24 March 2011

Serikali kupanua mradi wa maji kahama Shinyanga

Na Daud Magesa, Mwanza

SERIKALI imesema itaboresha na kufanya upanuzi katika wa mradi maji wa Kahama-Shinyaga ili kukidhi mahitaji na kuondoa kero ya maji kwa baadhi ya
mikoa ya Ziwa na Magharibi (Mwanza, Shinyanga na Tabora).

Akifunga Maadhimisho ya 23 ya Siku ya Maji Dunia ambayo Kitaifa yalifanyika mkoani Mwanza juzi, Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Ghalib Bilal alisema serikali itaufanyia upanuzi mradi huo mkubwa ili kuondoa au kupunguza kero ya maji inayoikabili mikoa hiyo kwa sasa.

Alisema kupanuliwa kwa mradi wa Kahama-Shinyanga, kutawezesha wananchi wa miji ya Nzega, Tabora, Igunga, Kagongwa, Isaka,Tinde na Mhunze na vijiji 76 vya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora.

"Serikali inatarajia kupanua mradi wa maji wa Kahama-Shinyanga ili kuwezesha wananchi wa mikoa ya Tabora, Shinyanga na Mwanza kupata maji safi na salama na kuwapunguzia kero ya maji inayowakabili, na itaboresha chanzo cha maji cha Nyahiti wilayani Misungwi," alisema Dkt. Bilal.

Mradi wa Maji wa Kahama-Shinyanga ulitekelezwa na serikali ya awamu ya tatu na kugharimu kiasi cha bilioni 244 zote zikiwa ni fedha zilizotokana na mapato ya ndani (kodi) bila kutegemea wafadhili wa nje.

Alidai kuwa mwamko mdogo wa kutolinda miundombinu na dira za maji, husababisha wananchi kukosa huduma ya maji na hiyo ni changamoto kubwa inayoikabili sekta ya maji nchini.

Aidha kuhusu uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji makamu huyo wa rais alisema kuwa husababisha taharuki katika jamii na kushauri ulinzi na utunzaji wa vyanzo hivyo ambapo alisema kwamba kuzinduliwa kwa mradi mkubwa wa majitaka jijini Mwanza utaboresha huduma za wananchi na kuwataka wajitume na kulipia huduma ili udumu na uwe endelevu.

Alieleza kuwa ukuaji wa miji usiozingatia mipango miji na ongezeko la watu mijini hauwiani na miundombinu ya maji, hivyo kusababisha ugumu wa kupitisha miundombinu ya uondoaji wa majitaka na kutokana na gharama kubwa.

Alisema wananchi wengi hawajaunganishwa na mtadao wa majitaka, hali inayochangia uchafuzi wa maji, vyanzo vya maji na mazingira kwa kutiririsha majitaka.

"Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya maji katika kuleta maendeleo, serikali itajitahidi kukarabati na kuimarisha uwezo wa watumishi, miundombinu na kuzipa mamlaka vifaa stahili," alisema Dkt. Bilal

Pia alisema kiasi cha sh. 654 milioni kimetolewa na serikali, kuboreha na kutatua kero ya majisafi na mataka katika Jiji la Dar es Salaam. Fedha hizo zitatumika katika kuboresha huduma ya maji safi na uondoaji wa majitaka jijini humo pamoja na miji ya Bagamoyo na Kibaha mkoani Pwani.

Alisema mradi huo utaanza mwaka 2011 na kukamilika 2013 lengo likiwa ni kuwaondolea kero ya maji wananchi wa maeneo hayo ambao wanapata asilimia kati ya 50 na 60, huku huduma ya majitaka ikiwa ni asilimia 10 tu. Katika utekelezwaji wa mradi huo, bwawa la Kidunda litajengwa ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu 30 na utandazaji wa mabomba majisafi na majitaka na upanuzi wa mitambo ya majisafi na majitaka.

No comments:

Post a Comment