17 March 2011

CUF kuichongea CCM kwa wananchi

Na Peter Mwenda

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeandaa ziara ya kuwashukuru wapiga kura na kuishtaki Serikali ya CCM kwa wananchi kwa kile walichosema kuwa imeshindwa
kuboresha maisha ya wananchi wake.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Julius Mtatiro aliyewakilishwa na Katibu wa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Thomas Mongi alisema ziara hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Bw. Mongi alisema CUF itaeleze wananchi mambo mengi yakiwemo kukosekana kwa umeme wa uhakika, kupanda kwa gharama za maisha hasa za vyakula kuuzwa bei ya juu na kupanda kwa nauli.

Alisema CUF itaeleza wananchi kuhusu matatizo makubwa katika sekta ya afya, uhaba wa maji, ukosefu wa ajira, miundombinu mibovu ya barabara, reli na matatizo katika sekta ya elimu.

Alisema pia wataitaka Serikali ya CCM kuhakikisha kuwa mchakato wa Tume Huru ya uchaguzi unafanyika mapema bila kusubiri mchakato wa kupata katiba mpya ya nchi.

Bw. Mongi alisema ziara hiyo ni muhimu kwa wananchi wote na itatumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa CUF iko bega kwa bega na wananchi wote bila kujali itikadi.

Alisema CUF haijali rangi, dini wala kabila ili kuwaletea wananchi wa Tanzania ukombozi wa kweli wa kiuchumi na kijamii.

Bw. Mongi alisema ziara hiyo itakayoanza Machi 19 hadi Aprili 2, pia itajumuisha Kaimu Katibu Mkuu Bw. Mtatiro, wajumbe wa Baraza Kuu la uongozi wa Taifa, Kiongozi wa wabunge anayetokana na CUF Hamad Rashid na baadhi ya wabunge wa CUF.

Hivi karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilifanya mikutano na maandamano mikoani kwa malengo kama hayo, jambo ambalo limeshambuliwa na chama tawala na serikali yake kuwa walikuwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuindoa serikali madarakani kama ilivyofanyika katika nchi za Tunisia na Misri.

2 comments:

  1. CUF Acheni kuiga!!!! kama hamna jipya kaeni kimya msubiri uchaguzi 2015, mle pesa za dowans na ccm, tunajua nyie ni ccm no.2. Acheni wapambanaji chadema wafanye kazi yao , wala msijipendekeze. mnachotaka kufanya ni copy paste sera za chadema. shut up yuor mouth!!

    ReplyDelete
  2. ww changiaji wa kwanza acha uandawazimu siasa ndivyo ilivyo unategemea kwani wao hawahitaji wanachama au kufanya mikutano ukiuliza wanaiga chadema chaedema pak tuu na we pia nyau tu

    ReplyDelete