21 March 2011

Rais Shein kuongoza harambee ya Z'bar Heroes

Rehema Maigala

RAIS wa Zanzibar Dkt. Mohamed Shein Anatarajia kuongoza harambee ya kuchangia timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' itakayofanyika
Machi 26, mwaka huu katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort ya mjini Zanzibar.

Akizungumza na wandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Future Century Sports Limited, Helene Masanja alisema lengo la harambee hiyo ni kuendeleza soka la Zanzibar.

Alisema harambee hiyo itawakutanisha wadhamini wa kudumu ili waweze kuidhamini Zanzibar Heroes ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

"Katika siku za hivi karibuni timu ya Zanzibar imeshuka kiwango kutokana na wachezaji kukosa hamasa ya wadhamini, hali iliyosababisha ya wachezaji kushuka," alisema Masanja.

Alisema harambee hiyo lengo lake ni kukusanya zaidi ya Dola 200,000 za Marekani ambapo kiasi hicho kitasaidia kutengeneza timu na taratibu za kiutawala.

Mkurugenzi huyo alisema harambee hiyo itarushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport kupitia ving'amuzi vya DSTV ambapo Zanzibar itapata nafasi ya kuonekana ulimwenguni kote.

Alisema DSTV tayari imekwishaweka taratibu za mafundi hao kuwasili nchini kutoka katika tawi lake la Kenya.

Alizitaja kampuni ambazo zimethibitisha kudhamini timu hiyo ni Benki ya wananchi Zanzibar, Mamlaka ya Bandari Zanzibar, Shirika la Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na kampuni nyingine ya binafsi.

No comments:

Post a Comment