28 March 2011

Jela miezi sita kwa kuwatoroka polisi

Na Said Hauni, Lindi

MAHAKAMA ya Mwanzo ya Lindi mjini, imemuhukumu Mkazi wa Kata ya Jamhuri katika Halmashauri ya Manispaa hiyo, Said Mkamba (28) kifungo cha miezi sita jela, baada ya
kujaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 22 mwaka huu, na Hakimu wa Mahakama hiyo, Jackrin Mmari, baada ya mshtakiwa  kukiri kosa hilo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Mmari alimuuliza mshtakiwa kama ana sababu za msingi zitakazoishawishi mahakama hiyo isimpatie adhabu kali, ambapo aliiomba imuonee huruma, akidai ni mgonjwa kutokana na sehemu ya viungo vyake kuwekewa vyuma.

“Mheshimiwa Hakimu ninaiomba mahakama yako tukufu, inionee huruma kwani ni mbovu kutokana na sehemu zangu kama za miguu kuwekewa vyuma, kutokana na ajali ya gari
niliyokuwa nimeipata siku za nyuma,” alisema Bw. Mkamba.

Hakimu Mmari akitoa hukumu katika kesi hiyo
alisema anashindwa kukukubali utetezi wake huo, kwa kuwa hakuna vielelezo vinavyomuonesha mshtakiwa
alipata ajali siku za nyuma, hivyo akamuhukumu kifungo cha miezi sita Jela.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Bw. Mkamba ambaye ni fundi magari, akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Sokoine yeye na mwenzake Bw. Mohamedi Mshangani wakipatiwa matibabu alijaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi, lakini Jaribio hilo halikufanikiwa  baada ya madereva wa pikipiki waliokuwa wamepaki nje ya hospitali hiyo, kumzingira  kwa nia ya kumchoma moto.

Bw. Mkamba na Bw. Mshangani wanadaiwa  Machi 19 mwaka huu, saa nne asubuhi,walivunja ghala la zamani la magereza na kuiba vitu mbalimbali, ikiwemo
gea Boksi ya gari aina ya Isusu, ambayo hata hivyo thamani yake hakupatikana kufahamika mara moja.

Washtakiwa hao waligunduliwa na walinzi wa kampuni ya simu, ambao nao walitoa taarifa kwa askari polisi wa Kituo cha Lindi mjini na kufanikiwa kuwakamata.

No comments:

Post a Comment