04 March 2011

pambano la watani wa jadi

*Simba, Yanga zatimua wachezaji

Na Elizabeth Mayemba

IKIWA imesalia siku moja, kabla ya miamba ya soka nchini Simba na Yanga kuvaana katika mechi ya Ligi Kuu mzunguko wa pili klabu hizo kila moja
zimetimua wachezaji kwa utovu wa nidhamu.

Klabu hizo kwa nyakati tofauti ziliwatumua wachezaji wake wa kuaminiwa ambapo Simba, amemzuia kiungo wake mahiri Mohamed Banka, huku Yanga ikimtimua mchezaji wake raia wa Ghana Ernest Boakye.

Habari ziliopatikana Dar es Salaam jana kutoka ndani ya kambi ya Simba iliyopo Zanzibar, zilidai kuwa Banka alitimuliwa baada ya kutoroka kambini siku moja kabla ya kupambana na Mtibwa Sugar.

"Ni kweli Banka hayupo kambini kwa kuwa alitimuliwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na ndiyo maana karibu mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara, hakupangwa," kilieleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kilidai kwamba uongozi wa Simba, umekuwa makini mno katika suala zima la nidhamu kwa wachezaji ambapo mara kwa mara wamekuwa wakipata ripoti kutoka kwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri.

Wakati huo huo habari kutoka ndani ya kambi ya Yanga, iliyopo Bagamoyo zinaeleza kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe amemuondoa Boakye katika kikosi kitakachoivaa Simba Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu bara, kutokana na utomvu wa nidhamu.

Yanga ambao juzi iliondoka jijini Dar es Salaam na kwenda kupiga kambi mjini Bagamoyo, Pwani kwa ajili ya mchezo huo, imeondoka na kikosi kizima isipokuwa kiungo huyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka kwa kiongozi mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alilithibitishia gazeti hili kwamba Boakye hajakwenda Bagamoyo kutokana na utomvu wa nidhamu.

"Wakati kocha Timbe akitangaza wachezaji watakaokwenda huko jina la Ernest (Boakye), halikuwepo kitendo ambacho kilizua maswali mengi lakini baadaye Timbe, aliwaondoa hofu kwa kusema anajua kwanini amemuacha," kilisema chanzo hicho.

Kiliendelea kusema kwa mujibu Timbe, kiungo huyo amekuwa mstari wa mbele kuwashawishi wachezaji wenzake kugomea mazoezi kwa madai ni magumu mno tofauti na waliyoyazoea.

Kilisema hiyo si mara ya kwamba kwa kiungo huyo kuzusha mambo yasiyo ya msingi kwani kuna wakati alisingizia kuumwa wakati timu ilipocheza na Azam FC Mkoani Tanga na uongozi uliamua kumrudisha jijini.

Akizungumzia sakata hilo Ofisa Habari wa timu hiyo, Louis Sendeu alikiri kiungo huyo kuachwa lakini akidai kwamba ni majeruhi.

3 comments:

  1. Lunyasi and yeboyebo tunataka mtuonyeshe soka la hadhi yenu kwani nyie ndio kioo cha soka la bongo, dakika 90 ziamue nani mmbabe na si vinginevyo. Sisi watazamaji tunalipa pesa ili tuone soka na si madudu.

    ReplyDelete
  2. Hao ndio wanaoharibu soka ya Bongo hakuna kitu!

    ReplyDelete
  3. Tena ndiyo wanaotutia aibu kwenye mashindano ya kimataifa,si kioo cha jamii bali ni aibu katika jamii.

    ReplyDelete