Na Mwandishi Wetu
BENDI ya muziki wa dansi ya Kalunde, imepata vyombo vipya vya kisasa ambavyo vitaanza kutumika kuanzia leo katika Ukumbi wa Mbalamwezi
uliopo Mikochezni, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Rais wa bendi hiyo, Deo Mwanambilimbi alisema vyombo hivyo viliwasili wiki iliyopita na leo mashabiki wa Kalunde wataanza kupata uhondo wa uhakika.
Alisema ujio wa vyombo hivyo ndiyo mwanzo wa kuingia katika ushindani wa muziki, kwani kwa muda mrefu bendi yake ilikuwa ikitumbuiza kwenye hoteli za kitalii.
"Kwa kweli tunatakwa kuwapa vitu vya nguvu mashabiki wetu, na kwa kuanzia leo tutawapa burudani ya kukata na shoka katika Ukumbi wa Mbalamwezi pale Mikocheni," alisema Rais huyo.
Alisema mashabiki watakaofika katika ukumbi huo, watapigiwa nyimbo zilizotamba mwaka jana pamoja na mpya ambazo zinatesa katika kumbi mbalimbali wanazopiga.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazorindima katika ukumbi huo leo ni pamoja na Nataka kuzaa na wewe, Itumbangwewe, Sisee, Fikiria, Nyemo, Hilda na Masumbuko.
Mwanambilimbi alisema pia bendi hiyo hiyo itakwenda mikoani kwa ajili ya utambulisho kwa mashabiki wake, ambao mara kadhaa wameomba Kalunde ipeleke sebene lake ili wakalicheze.
No comments:
Post a Comment