Na Zahoro Mlanzi
LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara, inaendelea leo kwa kupigwa michezo minne katika viwanja tofauti huku macho na masikio yataelekezwa katika Mikoa ya
Ruvuma na Dodoma.
Mashabiki wa mikoa hiyo pamoja na Arusha, watakuwa na kiu kubwa ya kujua hatma ya timu zao za Majimaji kutoka Songea na Arusha FC kutoka Arusha ambayo itasafiri mpaka mkoani Dodoma kuumana na Polisi Tanzania.
Kiu hiyo inatokana na nafasi za timu hizo katika msimamo wa ligi hiyo, ambapo Majimaji ipo nafasi ya pili kutoka mkiani kwa pointi 13 na Arusha FC ni ya mwisho ambayo ina pointi 11.
Majimaji na AFC zikipoteza michezo hiyo moja kwa moja zitakuwa zimejikatia tiketi ya kushuka daraja, kwani zitabakiwa na mchezo mmoja ambao hata zikishinda hazitaweza kuipiku timu iliyo juu yao.
Ruvu Shooting ipo nafasi ya 10, mbele ya Majimaji na AFC ikiwa na pointi 16, hivyo hata ikipoteza mchezo wao wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar bado wana nafasi ya kubaki Ligi Kuu kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Mchezo mwingine utapigwa jijini Dar es Salaam ambapo African Lyon itaikaribisha Toto African kutoka Mwanza katika mchezo ambao ni wa kukamilisha ratiba, kwani timu zote hazina cha kupoteza.
Msimu ujao wa ligi hiyo, timu mbili zitashuka na tayari timu zimepanda ambazo ni Villa Squad, Moro United za Dar es Salaam, Oljoro kutoka Arusha na Coastal Union ya Tanga.
No comments:
Post a Comment