16 March 2011

Mgosi, Tegete, Machaku nje Taifa Stars

*Poulsen awakumbuka Dihile, Kazimoto

Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Jan Poulsen amewatema katika kikosi chake wachezaji Mussa Hassan 'Mgosi', Jerry Tegete, Godfrey Bonny na
Salum Machaku, na kuwarudisha Mwinyi Kazimoto na Shaban Dihile.

Stars inatarajiwa kushuka uwanjani Machi 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam kucheza mechi ya tatu ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, zitakazofanyika katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon mwakani dhidi ya Afrika ya Kati.

Akitangaza kikosi hicho chenye wachezaji 23 Dar es Salaam jana, alisema kwa upande wa makipa amewaita Shaaban Kado, Juma Kaseja na Dihile, mabeki ni Shedrack Nsajigwa, Aggrey Morris, Nadir Haroub 'Cannavaro, Stephano Mwasika, Haruna Shamte, Juma Nyosso na Idrissa Rajab.

Viungo ni Nurdin Bakari, Shaban Nditi, Jabir Aziz, Henry Joseph, Abdi Kassim na Kazimoto, washambuliaji ni Nizar Khalfan, Dan Mrwanda, Mrisho Ngassa, Mohammed Banka, Athuman Machupa, John Bocco na Mbwana Samatta.

Wachezaji wengine waliotemwa ambao waliitwa wakati timu hiyo ikicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Palestina ni Chacha Marwa, Julius Mrope na Kelvin Yondan.

Poulsen alisema wachezaji aliowaita walimridhisha walipokuwa wakizichezea timu zao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, na ataendelea kufanya hivyo kila atakapokuwa akiita timu ya taifa.

"Wachezaji wote niliowaita wana ujuzi wa kutosha hivyo ninaamini watafanya vizuri katika mchezo wetu na Afrika ya Kati, lengo letu ni kucheza fainali za michuano hiyo,tulianza vizuri na tunatakiwa kumaliza vizuri," alisema Poulsen.

Kwa wachezaji aliowatema Poulsen alisema hawakumfurahisha katika mechi zao za ligi, na kila siku alikuwa akifuatilia michezo ya ligi ili kupata kikosi kizuri kwa ajili ya michuano hiyo.

Alisema pamoja na kwamba, Kado yupo katika kikosi cha timu ya Vijana Stars (U23), ameamua kumwita kwa kuwa Stars ni timu A na hiyo ya vijana ni timu B, hivyo mchezaji huyo anatakiwa kujiunga na timu A ambayo ni Stars.

Kocha huyo alisema timu yake inatarajiwa kuingia kambini kesho kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo huo, hivyo amewataka wachezaji wote aliowaita kuripoti kambini na kuanza mazoezi mara moja.

4 comments:

  1. Tanzania mpira bado mko nyuma na kinachosababisha ni ulaji wa viongozi wana tamaa na uroho wa fetha ndio maana unaona club hazina maendeleo.

    ReplyDelete
  2. Kichwa cha mwendawazimu sasa jina jipya sikio la kufa halisikii dawa ndio timu ya tanzania.

    ReplyDelete
  3. Poulsen hana jipya kaja kula pesa akimaliza mkataba wake onaondoka kama wengine walio mtangulia

    ReplyDelete
  4. Timu ya taifa ya Tanzania kila mwaka inakuwa na sura ipya na hata mwaka pia unnkuwa ni mkubwa.Hivi hao wachezaji wanaobadilishwa kila kukicha watazoeana saa ngapi?Nafikiri sasa ni wakati muafaka kuwa na vijana wadogo ambao wataendelezwa kwa muda mrefu na kuwa na timu iliyopamoja kwa muda mrefu kwani ninacho ona hapa ni kila baada ya mechi mbili au tatu timu inabadilishwa sasa tutafika mbali kweli?
    Maana tunakuwa na watu ambao hawajui nini wanafanya.Maana naona viongozi wa mpira Tanzania wako makini sana hasa kwenye viingilio vya mpira hasa wakati wa mechi kubwa badala ya kuwa na mikakati ya kudumu kuendeleza mchezo wa soka nchini.

    ReplyDelete