28 March 2011

Mosha arejea tena Yanga

*Atamba kuipa ubingwa wa Bara

Na Addolph Bruno

WANACHAMA wa Yanga jana wamekwenda nyumbani kwa Makamu wa klabu hiyo aliyejiuzu hivi karibuni, Davis Mosha kushinikiza
arudi madarakani kwa kuwa wao ndiyo waliomuweka madarakani na bado wanamtambua kikatiba.

Mosha alijuzulu wadhifa huo kwa madai ya kudhalilishwa na baadhi ya wanachama ambao walidai kuihujumu timu hiyo katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara.

Katika harakati hizo za kumrudisha Mosha madarakani zilifanywa na wanachama wa matawi 11 ya klabu hiyo, ambao walikwenda nyumbani kwake Mikochezni, Dar es Salaam ambaye waliondoka naye hadi makao makuu ya klabu hiyo katika mitaa ya Twiga na Jangwani.

Wanachama waliofika nyumbani kwa Mosha ni kutoka katika matawi ya Yetu Afrika la Kinondoni Hananasifu, Magomeni Makuti, Mtambani la Vingunguti, Kariakoo, Tandale sokoni na Msisiri.

Walidai kuwa sababu iliyowafanya wafikie hatua hiyo ni kwa kuwa bado wanamhitaji Mosha, kuendelea kuiongoza Yanga na wao bado wanatambua kuwa ni kiongozi wao kikatiba kutokana na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, kusahindwa kutoa tamko juu ya barua ambayo Mosha aliwaandikia.

"Tunashukuru kukukuta ukiwa katika afya njema, sisi ni wanachama wa matawi mbalimbali wa Klabu ya Yanga wenye mapenzi ya dhati na Yanga, tumekuja hapa kukuomba tuondoke kwenda katika klabu yetu," alisema mmoja wa wanachama hao aliyejitambulisha kwa jina la Mjaid Omari wa tawi la Furaha ya Yanga.

Alisema wanakubaliana na sababu za msingi ambazo Mosha, alizieleza katika barua yake ya kujihudhulu na kuongeza kuwa tatizo linaloendeleza migogoro ndani ya klabu hiyo linasababishwa na mmoja wa viongozi ambaye anakiuka katiba ya klabu na kwamba wanashangazwa na viongozi wengi kujiudhulu katika uongozi huu.

"Mpaka sasa tumewapoteza viongozi makini wengi sana na umefika wakati tujiulize, Kocha wetu Papic (Kostadine), Katibu Lawrence Mwalusako, Meneja Emanuel Mpangala, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na leo Makamu? nasema tatizo lipo lazima tukae tulijadili," alisema mmoja wa wanachama tawi la Uhuru aliyetambulika kwa jina la Said.

Hata hivyo Mosha aliwaambia wanachama hao asingeweza kukubaliana nao mara moja na kuwataka wampe muda wa siku mbili, akae na kupata ushauri kutoka katika familia yake lakini wanachama hao walipingana naye na kumwambia wangeweza kulala hapo kwa muda wa siku hizo huku wakipiga kelele.

Kutokana na msimamo wa wanachama hao, Mosha alikubali kuzungumza na familia yake na hatimaye kukubali kwenda katika klabu hiyo, ambako alizungumza na wanachama hao pamoja na wazee waliotumia muda mwingi kumshinikiza na yeye kuwahakikishia amekubali kuendelea na wadhifa huo kwa sharti la kuwataka wanachama kuendeleza umoja na mshikamano katika matawi yao.

"Mimi naipenda sana Yanga ndiyo maana natumia gharama kubwa katika kuhakikisha tunafanya vizuri, nilipoingia madarakani niliwaahidi nitamfunga mnyama (Simba) na nimefanya hivyo mechi mbili na kutoka sare moja, ila kuna watu wachache wananisumbua na kwa sababu mimi naipenda Yanga nikaona nikae pembeni," alisema Mosha.

Alisema atatumia nafasi hiyo kuhakikisha anaipatia ubingwa timu yake kwa kushinda mechi tatu zilizosalia ambazo ni dhidi ya Azam FC, unaotarajiwa kuchezwa Alhamisi katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa kuwa yeye ana uwezo wa kuwa na mipango.

No comments:

Post a Comment