16 March 2011

CHADEMA: Hatumlipi yeyote kuandamana

Na Peter Mwenda

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesikitishwa na kauli kinazodai ni propaganda za CCM kuwa kinatumia fedha kuwalipa wananchi
kuandamana.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Bw. Antony Komu alisema chama hicho haimlipi yeyote kuandamana, haijafanya wala haitafanya hivyo kwani wanaamini kuwa maandamano hayo ni harakati za wananchi kudai haki zao.

"Kwetu sisi haingii akilini kuwa yupo mwananchi anayeweza kufikiria kulipwa ili adai haki zake, tunasisitiza kuwa tutaendelea kuratibu maandamano haya nchi nzima," ilisema taarifa ya Bw. Komu.

Alisema Chadema itachukua maoni yote yanayotolewa katika maandamano na mikutano wanayofanya kwa kuwa ni maoni ya wenye nchi yao na ni lazima yasikilizwe na serikali yoyote inayotaka uhalali kwa watu wake.

Alisema uvumi mwingine unaoenezwa kuwa Chadema inapewa fedha na mataifa ya nje kuendesha maandamano kwa lengo la kuvunja amani hayo ni mawazo yenye lengo la kukidhoofisha chama hicho.

Alitoa wito kwawa wale ambao maandamano hayajafika kwao kujitokeza kwa wingi na kwa amani siku yakiwafikia, huku akiwataka kukwepa mtego wa wanaotaka kufanya fujo kuchafua mpango huo.

Bw. Komu alisema ili kuthibitisha kauli za mawaziri watatu kuwa Chadema inawalipa watu kuandamana zifanyiwe kazi na Jeshi la Polisi ili kupata ukweli wa tuhuma zilizoelekezwa kwa Chadema.

Alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Sophia Simba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Bw. Stephen Wassira kudai kuwa Chadema inalipa wananchi fedha kufanya maandamano ni upofu.

Alisema inashangaza kuona Idara ya Usalama wa Taifa, Polisi na Majeshi yahusike kupata ukweli badala ya kukaa kimya wakati kauli hizo zinayumbisha watu na kuiletea Tanzania maswali mbele ya jamii ya kimataifa.

Bw. Komu alisema Chadema inaona kuwa wao ni wazalendo wanaoipenda nchi na kuitaka iongozwe vizuri na watu wenye hadhi na mapenzi ya nchi na watu wake.

2 comments:

  1. Chadema endeleen na Maandamano ss wenye nchi tupo nyuma yenu hao mawaziri n waongo kwa sabab wao kwenye kampen zao walikuwa wanawalpa watu hela na kuwapa watu tishet PEOPLE'S POWER!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  2. Wenye nchi tunasema tutaendelea kusema ukweli na tutaendelea kuandamana hadi watuelewe...ujue ukiwa umezoea kufanya hivyo wanajua wote wanafanya hivyo...hatuhitaji kulipwa ili tuandamane...ccm wamezoea kuwalipa wananchi ili wawasikilize wajinga kweli

    ReplyDelete