17 March 2011

HUIWA kujenga kituo cha watoto yatima

Na Elizabeth Mayemba

KITUO cha Huduma ya Injili kwa Watoto Yatima (HUIWA), kimepanga kufanya matamasha mikoani kwa ajili ya kukusanya fedha za ujenzi wa kituo cha
watoto yatima ambacho kitagharimu sh. milioni 120.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mchungaji wa kituo hicho, Maximilian Machumu alisema katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika wamepanga kufanya matamasha katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Tanga.

"Lengo letu kubwa ni kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kitakachogharimu sh. milioni 120 katika hatua za awali, na maandalizi ya ujenzi huo yameanza kwa kumpata mtaalamu ambaye anafanya tathmini ya ujenzi wa kituo hicho," alisema Machumu.

Mbali ya matamasha hayo, alisema pia wamepanga kutoa albamu itakayobeba jina la Nani atakwenda badala yake,  ambayo itakuwa na nyimbo nane zinazoelezea na kuhamisha watu, makanisa na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali kusaidia na kuwajali watoto yatima popote walipo nchini.

Alisema albamu ya kwanza iliyobeba jina la Bonde la kukata maneno, waliizindua Machi 6 mwaka huu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Monduli Edward Lowasa.

Mchungaji huyo alisema atawawekea mikono ya baraka na kuwaombea wale wote waliotoa michango yao, katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho ili pale walipopungukiwa, Mungu azidi kuwaongezea vipato vyao na kuwabariki.

No comments:

Post a Comment