25 March 2011

Maamuzi mabovu yapoteza bilioni 20/- za serikali

Na Tumaini Makene

KITENDO cha Wizara ya Maliasili na Utalii kuingilia maamuzi ya Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kimeligharimu taifa takribani sh. bilioni 20 ambazo
zingepatikana kupitia tozo kutoka kwa hoteli za kitalii nchini katika mwaka wa fedha 2009/10.

Maamuzi ya Bodi ya TANAPA yaliyoingiliwa na uongozi wa wizara hiyo yalikuwa ni kushusha viwango vya malipo wanayostahili kulipa wawekezaji wa hoteli hizo, kutoka dola 20-50, hadi dola 3-15, hali ambayo pia imesababisha kushuka kwa mapato kutoka bilioni 21 kwa mwaka kufikia bilioni 1.5.

Hayo yaliibuliwa jana katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambapo baadhi ya wabunge walihoji sababu ya kushuka kwa mapato ya shirika hilo, kama ilivyooneshwa katika Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hii itakuwa mara ya pili kwa wizara hiyo kupindisha mambo, kwa maslahi ya wawekezaji wa sekta ya utalii, badala ya maslahi mapana ya taifa.

Aliyeanza kuibua hoja hiyo iliyozua mjadala, alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Mwibara, Bw. Kangi Lugola, akisema kuwa ripoti ya CAG imebainisha TANAPA wanatoza ada ndogo kwa wawekezaji wa hoteli za kitalii ndani ya mbuga za taifa, hivyo kushusha mapato ya shirika hilo la umma na taifa kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Bw. Allan Kijazi alijibu kuwa awali Bodi ya TANAPA iliweka viwango vya malipo kwa wawekezaji hao kwa ada ya dola 20-50, lakini wamiliki wa hoteli kupitia chama chao (HAT) walizipinga. 

Kwa mujibu wa Bw. Kijazi, pingamizi hilo lilikubalika kwa waziri, hivyo akaamua kuingilia na kuwaagiza TANAPA, kuacha kutoza kodi hizo mpya, badala yake washushe viwango hivyo, mpaka dola 3-15.

Alisema kuwa wao hawana budi kutekeleza agizo la waziri mwenye dhamana, badala ya uamuzi wa bodi.

Wabunge kadhaa waliochangia walihoji mamlaka aliyonayo waziri wa wizara husika kuingilia maamuzi ya bodi ambayo inahusisha wataalamu katika suala la kupandisha tozo kwa wawekezaji hao.

Akizungumza na Majira nje ya kikao, Mwenyekiti wa POAC, Bw. Kabwe Zitto, alisema kuwa sheria zinazosimamia mashirika ya umma bado zina utata, hasa katika majukumu ya waziri, kwani zinamruhusu kuliagiza shirika, nalo linapaswa kufuata maagizo hayo, lakini akahoji;

"Sasa nini maana ya kuwa na bodi yenye wataalamu, ambayo imeteuliwa na kuaminiwa na waziri huyo huyo...sasa tumebatilisha uamuzi huo wa waziri, kuanzia sasa TANAPA watatoza ada kama ilivyoelekezwa na bodi...we are sending a message to all ministers (huu ni ujumbe kwa mawaziri wote) kuwa wafanye kazi wakijua kuna chombo kinawaangalia na kuwasimamia kama inavyoelekezwa katika ibara ya 63 ya katiba".

Akizungumza katika kikao hicho, mmoja wa wajumbe wa bodi ya shirika hilo, Dkt. Macelina Chijoliga, alisema kuwa watafayanyia kazi maamuzi ya kamati hiyo ya POAC, kwa nia ya kuboresha sekta ya utalii nchini inufaishe taifa.

Wakati huo huo, wabunge katika Kamati ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, wameonekana kutoa tahadhari juu dhamira ya dhati kwa nchi wanachama katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakisema kuwa maslahi ya Tanzania na Watanzania yanapaswa kupewa uzito unaostahili.

Takribani wabunge wote waliochangia katika mjadala wa jana ambapo kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Bw. Edward Lowassa, ilikuwa ikipokea na kujadili taarifa ya wabunge wa bunge la Afrika Mashariki, walionekana kuhoji namna gani Tanzania itaweza kunufaika na ushirikiano huo, hasa katika hatua ya soko la pamoja.

Bw. Lowassa alihoji suala la wageni wanaonunua ardhi 'kwa fujo' hasa katika maeneo ya Mkoa wa Arusha na mingine ya jirani, wakati suala hilo halimo katika moja ya makubaliano ya jumuiya hiyo. Alitaka kupata ufafanuzi pia kutoka kwa wabunge hao iwapo hatua ya shirikisho la kisiasa kwa jumuiya hiyo inawezekana.

Bw. Lowassa pia alihoji kwa nini Kenya wanajenga uwanja wa ndege mkubwa karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), hali ambayo imekuwa ikisemwa kuwa 'itahatarisha' hatma ya KIA, wakati nchi hiyo ilipaswa kuzingatia kuwa nchi hizo mbili ziko ndani ya ushirikiano.

"Naona sasa hivi wananunua viwanja vingi tu huko jirani zetu sasa...lakini pia kama tuko katika ushirikiano pamoja ya nini kuwa na uwanja wa ndege karibu na KIA, na wengi wa wanaharakati wanaopinga unjezi wa barabara ya Serengeti ni Wakenya," alisema Bw. Lowassa.

Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Isarel Natse alitaka kujua namna gani wabunge wa bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania walivyo makini katika kuhakikisha maslahi ya nchi yao yanazingatiwa wanapokuwa katika vikao vya bunge hilo, akisema Tanzania inapaswa kuwa makini 'tusije tukajikuta tunashikwa masikio', akisema nchi zingine zinaonekana kujipanga vilivyo.

Mbunge wa Ilala (CCM), Bw. Mussa Zungu alitaka kujua ilikuwaje Kenya kama mmoja wa nchi wanachama wa EAC, ilipinga na kisha ikafanya kampeni ya kuhamasisha nchi zingine ziipinge Tanzania kuuza pembe za ndovu mwaka jana, kisha imekuwa ikihamasisha wanaharakati kupinga ujenzi wa mahoteli ya kitalii na barabara katika maeneo ya mbuga za Tanzania.

Suala jingine lililotatiza kikao hicho ni upashaji habari kwa umma mkubwa wa Watanzania juu ya fursa zilizopo na namna gani mambo yanaendeshwa katika ushirikiano wa jumuiya hiyo, hali iliyomfanya Bw. John Chiligati kusema 'iko siku tutajikuta ndani ya shirikisho la kisiasa bila hata kujua'.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dkt. Fortinatus Masha, alisema kuwa manung'uniko na hoja zote walizotoa wabunge wa bunge la Tanzania zilikuwa ni za kweli, ingawa zingine zilielekezwa mahali sahihi (kwa wabunge hao) lakini nyingi zilipaswa kuulizwa kwa serikali, akisema mambo mengi yamekuwa yakiamuliwa na serikali za nchi wanachama kabla hayajafikishwa katika bunge hilo.

3 comments:

  1. Kwenda kwa Mkurugenzi Manispaa ya Ilala.
    Ufisadi huu hadi lini Ofsi ya Maji Ilala.
    Inashangaza kuwa watu wachache ndio wanaokula pesa kizembe tu ofsi ya maji ikiongozwa na Fisadi namba moja Selestina Magesa, na group lake Opitaty Kwembe mtu alie na darasa la kwanza ila wizi anaujua kupta mtu yeyote, pamoja na Wilfred Kavishe, Alex Odena, na Kahema amekuja ofsi ya maji kuja kuiba vzr pesa za miradi ya maji maana kahema na Optaty kwembe ni mahawara waliobobea! Mkurugenzi tunapenda kukutaarifu kuwa pesa ya wiki ya maji haijafaya kazi yoyote kwani baadhi ya madiwani walichoshwa na upuuzi wa viongozi hawa wa ofis ya maji na kususia uzinduzi wa wiki ya maji visima havina ubora na pia miradi mingi ni hewa tunakuomba utoe samaki wabovu ofisi ya maji ili ili kuwasaidia warengwa wa miradi husika. Tunashangaa kuona kuwa huyu kahema kaja kinyemera ofisi ya maji kisa ni mpenzi wa Optaty kwembe tunashangaa pia kuona kisima cha depot kuchimbwa kwa miliion 9 badala ya million 5, na kisima hakina ubora wa utoaji maji ya kutosha pia watumishi hapo depot bwanakosa maji vyooni na hakuna anaelishughulikia swala hili.
    TUTAENDELEA KUKUPA TAARIFA ZAIDI KUHUSU UOZO WAO NA TUNAOMBA UWAKALISHE NA KUWATIMUA IKIBIDI KWANI HAWANA NIA NZURI NA MATAKWA YA SERIKALI ZAIDI YA KUJINUFAISHA WAO TU.

    ReplyDelete
  2. Hii comment ya Maji Ilala hapa si mahali pake

    ReplyDelete
  3. Waziri husika achululiwe hatua au ajiuzulu maana hana mamlaka kubwa kiasi hicho. utoto alionao asilete ktk kazi.

    ReplyDelete