29 March 2011

Deni TANESCO laishtua Kamati ya Bunge

Na Tumaini Makene

DENI linalokadiriwa kuwa kati ya sh. bilioni 67 na 96 linaloonekana kulielemea Shirika la Umeme nchini (TANESCO) umeishtua Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mahesabu ya
Mashirika ya Umma (POAC) na kulazimika kuiita wizara za Nishati na Madini pamoja na Fedha na Uchumi, kujadili kwa kina suala hilo.

Habari hizo zimekuja wakati ambapo Kwa muda mrefu sasa imekuwa ikidaiwa kuwa shirika hilo limeelemewa na mzigo mkubwa wa madeni, unaoliweka katika hali mbaya kiuchumi kiasi cha kushindwa kukopesheka, huku mapato yake kwa mwezi yakiwa hayaendi sambamba na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Bw. Murtaza Mwangunga alisema kuwa wajumbe wa POAC walishindwa kupitisha hesabu za TANESCO mpaka watakapopata maelezo ya kina juu ya deni hilo kutoka wizara hizo mbili.

"Wizara hizo mbili yaani ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Fedha na Uchumi zitakuja hapa, tumeagiza watendaji wake, makatibu wakuu wa wizara hizo waje hapa siku ya Jumatano, ili tujadili kwa kina sababu ya tatizo hilo," alisema Bw. Mwangunga.

Akizungumza kwa tahadhari akisema kuwa hataki kuiingia kwa kina katika suala hilo, kiasi cha kuathiri kanuni za bunge, alisema kuwa inaonekana hakuna taarifa za kutosha, hasa uhusiano kati ya taarifa za wizara hizo mbili na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

"...hata TANESCO wenyewe wako puzzled (wanashangaa) hawajui nature ya madeni haya yanayokadiriwa kuwa kati ya sixty seven bilion hadi ninety six bilion shillings, wameshindwa kuyatolea maamuzi," alisema Bw. Mwangunga, akisisitiza hawezi kusema masuala mengi kwa kina mpaka watakapoweza kusikiliza pande zote husika.

Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetangaza 'hali ya hatari' ikisema kuwa haitaachia uozo unaoendelea katika halmashauri za wilaya hasa katika ufisadi wa fedha za serikali, ambapo zimekuwa zikitumika vibaya katika matumizi 'feki'.

Akitangaza hilo jana mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa LAAC, Bw. Agustine Mrema alisema "ama zao ama zetu...haponi mtu hapa", akisema kuwa kamati hiyo imemwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu kwa baadhi ya halmashauri za wilaya zilizoonekana kutapanya fedha katika maeneo kama vile manunuzi na mishahara hewa.

Alisema kuwa katika wilaya takribani kumi pekee ambazo zimeitwa na kamati hiyo, Rorya, Kilosa, Morogoro, Rungwe, Mbeya, Sumbawanga, Msoma Vijijini, Tarime na Kisarawe, kumegundulika upotevu wa sh. milioni 792 katika mwaka mmoja wa fedha 2008/209, kwa kuwalipa wafanyakazi ambao hawapo.

"Tulichokiona ni kuwa kuna uozo mkubwa ndani ya halmashauri, hasa katika suala la mishahara hewa, fedha za serikali zinatumika kulipa watu waliokwisha kufa, watoro ambao hawako kazini, wengine walikwisha fukuzwa siku nyingi, hili ni jambo linalotisha.

"Mambo haya si kwamba hayafahamiki, yanafahamika sana, wapo watu wanahosika kuidhinisha malipo hayo, kwa mfano Wilaya ya Morogoro wametumia sh. milioni 19.4 katika mishahara hewa...Serengeti milioni 39.4, Tarime milioni 89.1, Kilosa 84.1," alisema Bw. Mrema.

Alisema kuwa wameagiza uchunguzi maalumu wa CAG ufanyike, kisha taarifa zitolewe kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili wahusika wachukuiwe hatua za kisheria, ikiwemo kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment