08 March 2011

LAAC yaagiza watendaji Same kukatwa mshahara

Na Martha Fataely,Same

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),imeagiza Mkurugenzi wa wilaya hiyo,Bw Joseph Mkude na wakuu wa idara wilayani humo,kukatwa
asilimia 15 ya mishahara yao agizo lililokwenda sambamba na kupewa onyo kali baada ya kubainika kwa uzembe na uandaaji mbaya wa taarifa za fedha.

Kamati hiyo iliyoanza kazi rasmi mkoani Kilimanjaro,chini ya mwenyekiti wake,Bw. Augustine Mrema kabla ya kutoa uamuzi huo iliwatoa nje ya ukumbi kwa saa moja Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo,Bw. Athuman Mdoe na viongozi wote wa
halmashauri ili kujadiliana hatua za kuchukua.

Akizungumzia na viongozi baada kurejea,ukumbini,Bw. Mrema alisema kamati haijaridhishwa na taarifa za fedha kutokana na kukinzana katika suala la Mapato, Matumizi, michanganuo ya fedha na hesabu halisi zilizowasilishwa kwa mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali(CAG).

Mbele ya wajumbe wengine nane wa kamati hiyo,mwenyekiti huyo alisema kutokana na kuwapo kwa hesabu mbovu za halmashauri hiyo,kamati yake haitaweza kukagua tena miradi iliyokuwa imekusudiwa kwa kuwa itakuwa chini ya viwango.

“Lazima tufahamu kwamba hatukuja hapa kutembelea miradi,tumekuja kufanya ukaguzi wa hesabu na miradi…hizi taarifa zenu ya fedha ni Mbovu,pamoja na kuwa na wasomi lakini mmeshindwa kuandika taarifa,mtachukuliwa hatua kali za kisheria na barua za onyo,”alisema.

Bw. Mrema alifafanua kwamba adhabu hiyo haitamhusu Kaimu Ofisa Mipango wa halmashauri hiyo,Bw. Alfon Kavumo ambaye alihamishiwa katika Wilaya hiyo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

Alisema halmashauri hiyo imeshindwa kutunza kumbukumbu za hesabu huku ikiandika taarifa zinazotofautina kati ya zile CAG na nyingineambazo ni kumbukumbu za halmashauri.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Iddi Azan,alisema pamoja na hatua ambazo zimetangazwa lakini hatua zaidi za kisheria zitatangazwa hapo baadaye kutokana na mapungufu yaliyobainika.

Alisema miradi ambayo imebainika kuwa na mapungufu ni ya Maji, Afya, Barabara na Elimu ambayo matumizi yake ya fedha yanatofautiana kwa kati ya Sh Mil.50 hadi sh. mil.100  katika mapato na michanganuo ya fedha hizo.

Alisema taarifa kama hizo zinaashiria kuwapo kwa udanganyifu katika idara ya fedha na uzembe kwa uongozi wa halmashauri kwani hapakuwa na sababu za kuwapo kwa taarifa
zinazokinzana.

Kwa upande wake,Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo,Bw. Mdoe aliridhia kutolewa kwa adhabu hizo na kuahidi kushirikiana na mkurugenzi na wakuu wengine wa idara kufanya marekebisho ya udhaifu uliobainika.

No comments:

Post a Comment