24 March 2011

Kikwete atonesha kidonda TRL

Na Edmund Mihale

RAIS Jakaya Kikwete amesema haoji haja ya watumishi wa wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) wakiwamo wenye umri mkubwa kulipwa mkono wa heri na
kuajiriwa upya na endapo itafanyika hivyo, vigezo vya ajira vizingatiwe.

Rais Kikwete alisema hayo jana baada ya waziri wa wizara husika, Bw. Omar Nundu, kutoa maelezo ya utekelezaji wa maagizo aliyotoa rais mwaka 2006.

"Najua kuwa kuna watu wa maika 55 hadi 60 bado wapo kazini, angalieni hapo nao wanataka walipwe na kurudi kazini hapo mie sielewi," alisema Rais Kikwete.

Awali Bw. Nundu alisema kuwa serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi hao malipo ya uzeeni ili ajira zianze upya na kuongeza morali ya kazi kwa wafanyakazi hao jambo ambalo lilionekana kumshangaza Rais Kikwete.

Alisema kuwa ni jambo la ajabu kusikia watu wapo kazini lakini wanataka kulipwa malipo ya uzeeni. "Mimi sijui watu wapo kazini lakini wanataka waachishwe kisha waajiliwe upya katika kampuni hiyo hiyo hebu nielewesheni hapo nami nielewe kwani siwaelewi mnamaanisha nini kuhusu jambo hilo," alisema Rais Kikwete.

Kauli hiyo ilimpa wakati mgumu Bw. Nundu ambaye alionekana kupata kigugumizi kwa muda na kueleza kuwa wanachotaka wafanyakazi hao ni kupewa mkono wa heri baada ya wenzao walioachishwa na kupewa mkono wa heri kurudishwa kazini.

Rais Kikwete alisema iwapo wizara hiyo itafanya hivyo basi izingatie kanuni na sheria za ajira katika kuajiri upya wafanyakazi hao.

kwa muda mrefu wafanyakazi wa TRL wamekuwa wakiendesha migomo, pamoja na mambo mengine, wakishinikiza kupewa mkono wa heri, kulipwa mafao yao na kupewa mikataba mipya baada ya serikali kukodisha shirika hilo.

Mgogoro wa TAZARA

Rais Kikwete alimtaka, Bw. Nundu kuteua Naibu Mkurugenzi mwenye uwezo kwa kuongoza Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) kwa upande wa Tanzania ili kuepuka migogoro inayojitokeza sasa.

Awali Bw.Nundu alisema kuwa shirika hilo limekuwa na migogoro ya muda mrefu kutokana na mfumo wa uongozi uliopo katika shirika hilo, lakini Rais Kikwete aliingilia kati taarifa hiyo na kuuliza kuwa tatizo ni mfumo au kiongozi.

"Hapa sioni tatizo lenu nini hapa baada ya kuchagua kiongozi mzuri bali mnachagua kada hata makada wakati mwingine wanakuwa wazuri. Sasa mnamlaumu nani mfumo si tatizo bali mnawekana pale, mtu hana uwezo hawezi kuongoza manejimneti, Bw. Mfutakamba anatafuta mnyamwezi mwenzake naye anamwambia kuwa kaa hapa huu ndiyo wakati wetu anaongoza manejimenti," alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa tatizo si mfumo bali ni utaratibu wa watu kushindwa kuchagua mkurugezi anayefaa kuongoza chombo hicho na kumtaka Bw. Nundu kufanya hivyo.

Mmalaka ya Hali ya Hewa (TMA)

Rais Kikwete aliitaka mamlaka hiyo kumshirikisha katika mpango unaondaliwa ili kuuboresha.

Alisema kuwa imefika wakati wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa uhakika ili kutoa utabiri utakaomnufaisha mkulima mbaye amekuwa akiwekeza bila kujua ni lini mvua itanyesha na kupata hasara.

"Nataka mnimbie tufanyeje ili kuboresha mamlaka yetu na tuachane na utabiri wa mvua za mtawanyiko, za hapa na pale mara nyingine kutakuwa na mawingu sasa tuwe kama  wenzetu wa Marekani. Mnakumbuka alipokuja Rais Bush hapa wale jamaa walitabiri mvua itanyesha muda gani hadi saa walituambia kuwa tufanye mkutano wetu mwisho saa nne mvua itanyesha na ikawa hivyo," alisema Rais Kikwete.

Usafiri wa majini

Rais Kikwete alitaka wizara hiyo kuboresha usafiri wa majini kwa kuongeza kina katika Ziwa Tanganyika ili kuongeza mizigo katika bandari hiyo ambayo kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa.

"Pale Kigoma kuna meli ya Mv. Lihemba sasa Wajerumani wanajindaa kusherekea miaka 100 ya meli hiyo, imezeeka tunahitaji kupata meli mpya. Pale Ziwa Nyaza tangu ilipozama Mv. Mbeya mwa 1977 hakuna meli nyingine kunahitajika kupata meli nyingine mpya lazima ipatikane. Nyingine ni ile ya Ziwa Victoria iliyozama tunahitaji kupata meli nyingine pia," alisema Rais Kikwete.

1 comment:

  1. ASANTE RAISI LAKINI TATIZO MANENO YAKO MATAMU NA MAZURI YENYE KUTIA MOYO, HAYATEKELEZWI NI BORA PIA UKAWAPA MUDA WA KUKULETEA MATOKEO SIO IISHIE HAPO TU MAANA KUSEMA NI RAHISI KULIKO VITENDO,WATENDAJI WETU NDIO MATATIZO HAWAWAJIBIKI IPASAVYO

    ReplyDelete