01 April 2011

Kikwete aahidi kuisadia Zimbabwe

Na Edmund Mihale

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Tanzania itaendelea kuisaidia Zimbabwe kutatua matatizo yake hasa yale ya kisiasa na pia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kutekeleza
majukumu yake.

Katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Bw. Morgan Tsvangirai yaliyofanyika Ikulu Dar es Slaam jana, Rais Kikwete alisema “Sisi katika Tanzania tunataka kuiona Zimbabwe yenye amani, yenye mafanikio na tuko tayari kusaidia kwa namna yoyote ambayo wananchi na Serikali ya Zimbabwe wanaona inafaa.

Bw. Tsvangirai ambaye aliwasili nchini juzi usiku akiwa amefuatana na maofisa saba, alimwelezea Rais Kikwete kuhusu hali ilivyo katika Zimbabwe na ushirikiano ulivyo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika nchi hiyo.

Ziara hiyo ya Bw. Tsvangirai katika nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ina lengo la kuwaelezea viongozi wa nchi hizo hali ilivyo Zimbabwe na changamoto zinazoikabili Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kabla ya kuja Tanzania, alikuwa ametembelea Malawi, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Namibia, Msumbiji, Afrika Kusini na Ufalme wa Swaziland.

Mara baada ya mazungumzo  hayo Bw. Tsvangirai na ujumbe wake waliondoka Dar es salaam kwenda Livingstone, Zambia kuhudhuria mkutano wa nchi tatu zinazounda Kamati Maalumu (Troika) ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC iliyokutana jana.

Kamati hiyo iliyoundwa Juni mwaka 1996 ndiyo yenye jukumu ya kujadili na kutafuta njia za kumaliza matatizo ya kisiasa katika eneo la nchi wanachama wa SADC na nchi tatu zinazounda Kamati hiyo kwa sasa ni Zambia, Afrika Kusini na Msumbiji.

Rais Rupiah Banda wa Zambia atakuwa mwenyekiti wa kikao hicho ambacho pia kinahudhuriwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Rais Armando Emilio Guebuza wa Msumbiji.

2 comments:

  1. "RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Tanzania itaendelea kuisaidia Zimbabwe kutatua matatizo yake hasa yale ya kisiasa na pia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kutekeleza
    majukumu yake."

    Mh toa boriti kwenye jicho lako kwanza alafu..... kwa jirani, Nyumbani kwako kumeoza kabisa

    ReplyDelete
  2. Ilikuwa ni April fool!

    ReplyDelete