01 April 2011

Kilango amshutumu DC kuingilia kazi zake

Na Martha Fataely, Same

HALI si shwari katika maendeleo ya Kiwanda cha Tangawizi wilayani Same, baada ya Mbunge wa Same Mashariki, Bi. Anne Kilango, kudai Mkuu wa Wilaya hiyo
, Bw. Ibarahim Marwa, anafanyakazi zinazodhoofisha juhudi za wakulima wa zao hilo.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani, Bi. Kilango alisema, Bw. Marwa ameteua kamati ya kusimamia ujenzi wa uzio na kibanda cha mlinzi kiwanda hapo ambayo ni kinyume cha taratibu, jukumu ambalo siyo lake na kuiacha bodi halali inayosimamia kiwanda hicho.

“Sipendi kumtaja mtu kama hayupo, nimesikitika kuona kwamba Mkuu wa Wilaya hayupo katika kikao hiki amekuwa akiingilia kazi zisizomuhusu,yeye kama kiongozi wa serikali hahusiki katika kuteua kamati ya kuendeleza ujenzi, nani kamtuma,” alihoji.

Alisema amehangaika na kiwanda hicho kwa zaidi ya asilimia 90 huku asilimia zilizobaki ni nguvu za wananchi na wahisani mbalimbali ikiwamo harambee iliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete ambapo zaidi ya sh milioni 285.9 zilipatikana.

“Nimepitisha bakuli kila mahali Rais Kikwete aliniambia niwe na sh milioni 100, nimekwenda mikoa mbalimbali kutafuta fedha hizo leo nimekwenda Kijiji cha Bwambo nauliza huu ujenzi mnaujua wanasema hawajui, kibanda chenye hakina kiwango,” alisema.

Alisema kitendo cha Bw. Marwa  kutoa kazi hiyo kwa mkandarasi kujenga uzio na kibanda hicho ni kuwatenga wakulima na wananchi wa vijiji vya Bwambo na Mamba ambao walishiriki mchakato mzima wa ujenzi tangu hatua ya msingi hadi sasa.

“Nimepata barua kutoka kwa DC eti tueleze jinsi ya matumizi ya fedha za michango ya ujenzi wa kiwanda hiki michango nitafute mwenyewe, nihangaike halafu aje mtu mwingine aulize natumiaje,naomba baraza lipitishe azimio kiwanda kirudi chini ya halmashauri na siyo Kamati ya Mkuu wa Wilaya,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Christopher Irira aliomba busara kutumika katika suala hilo kwani wapambanapo mafahari wawili ziumiazo ni nyasi na kwamba kabla ya kiwanda kurejeshwa kwa halmashauri kifanyiwe ukaguzi ili kujiridhisha kiko salama.

Hata hivyo baraza hilo lilipitisha kwa kauli moja azimio la kutaka kiwanda kiendeshwe chini ya bodi yake husika kwa usimamizi wa wataalamu wa halmashauri kama ilivyokuwa awali.

Akijibu hoja za Bi. Kilango, Bw. Marwa alisema hajaingilia uendeshaji wa kiwanda kama inavyodaiwa na pia hajateua kamati yoyote kusimamia ujenzi bali majukumu yote yanafanywa na Chama cha Wakulima wa Tangawizi kupitia bodi yao.

“Huyu mbunge amekurupuka katika hili anataka umaarufu wa kisiasa, kwanza anatakiwa ashukuru kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda…shughuli zote zipo chini ya bodi na wataalam wa halmashauri,mimi ni kiongozi wa serikali hapa ni msimamizi tu,” alisema.

Bw. Marwa alisema hajaunda kamati yoyote katika uendeshaji wa kiwanda wala kuteua kamati kama mbunge huyo anavyodai bali aliagiza timu ya msukumo wa ujenzi wa kiwanda hicho kuharakisha na kuendeleza ujenzi baada ya kusimama kwa muda.

“Nilipata malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu kusimama kwa ujenzi,nami kama kiongozi wa serikali niliiagiza bodi chini ya wataalamu wa halmashauri kuharakisha ujenzi huo jambo ambalo limefanyika…huyu Kilango anadandia hoja,hata wazo la kiwanda siyo la kwake ni kutoka serikalini,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi inayoendesha kiwanda hicho, Bw. Elisafi Kiariro, alikana madai ya Bi. Kilango kwamba shughuli za kiwanda kuendeshwa na Kamati ya Mkuu wa Wilaya bali bodi yake imekuwa ikishiriki kwa kila jambo.

“Ujenzi wa kiwanda umeendelezwa kwa ushirikiano na wataalamu wa halmashauri na bodi yake lakini pia tumeshirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri, Meneja wa Sido na Wawakilishi wa Uwezeshaji Faida mali hivyo hakuna jambo linalofanyika bila bodi yangu kujua,” alisema.

Alisema waliitwa na Mkuu wa Wilaya akiwa kama kiongozi wa serikali akitaka kufahamu maendeleo ya ujenzi wa kiwanda ambapo aliwaagiza kuharakisha ujenzi huo ili wakulima wanufaike kwa kuuza mazao yao .

“Mbunge wetu alifika katika kipindi cha kama wiki tatu au nne zilizopita na kutembelea kiwanda lakini alidai kutoridhishwa na ujenzi wa uzio ambapo alisema atakwenda kuzungumza wilayani sisi hatujui amekwenda kusema nini huko wilayani,” alisema.

4 comments:

  1. Hongera Mama Anne Kilango juhudi zako kama Mbunge zimeonekana mbona hapo zamani Kiwanda hakikujengwa? Mkuu wa Wilaya kutana na Mbunge ili mzungumze na kuelewana kwa manufaa ya wananchi,l acheni kauli za kusema kukurupuka, wote ni watendaji wa wananchi, fanyeni kazi kwa kujulishana na kuelewana, sisi wananchi tupo nyuma yenu tukitaka maendeleo.

    ReplyDelete
  2. HUYU MKUU WA WILAYA MARWA HUWA ANATUMIWA NA WATU WA KINA LOWASSA KUMDHOOFISHA MAMA KILANGO NA HII INAJULIKANA WAZI. SIO FAIR NA WPARE HATUTAKUBALI KAMWE. NDIYE MBUNGE TULIYEMTAKA NA KUMCHAGUA. AENDELEE KUPAMBANA NA UFISADI.

    ReplyDelete
  3. jamani ya same mnayajua au mnaongea tu ili kuongeza idadi ya comment hapa?? kitanda usichokilalia haujui kunguni wake so kama huna uhakika na mambo ni vizur unyamaze kuliko kulaumu bila kuelewa lipi ni lipi. Watu wanatafuta tu umaarufu hata pale pasipostahili. Kujengwa Kiwanda halikuwa wazo lililoanzishwa na Anne Kilango bali ni ni wazo la serikali ili kuwakwamua na kuwasaidia wananchi wa Mamba Myamba ambao wamekuwa wakilanguliwa kwny mauzo ya zao la Tangawizi. Huyu Anne analaumu tu bila kujua nn anaongea.

    ReplyDelete
  4. Marwa ni rafiki yangu sana, lakini hapo amechemka. Alikuwa amekunywa kidogo, maana namfahamu jamaa. Akinywa mambo si mabaya. POLE jamaa yetu.

    ReplyDelete