Na Elizabeth Mayemba
PAMOJA na Makamu Mwenyekiti wa Yanga aliyejiuzulu wadhifa huo hivi karibuni, Davis Mosha kukataa kujadiliwa uamuazi wake, Kamati ya Utendaji ya klabu
hiyo leo imepanga kumjadili.
Hivi karibuni Mosha, aliomba wanachama na viongozi wa klabu hiyo kutii maamuzi yake na kuacha kuendelea kumjadili katika vikao vyao.
Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema leo Kamati ya Utendaji mbali ya kujadili mechi tatu zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom, pia wataijadili na barua ya Mosha na kuitolea maamuzi.
"Leo Kamati ya Utendaji inakutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo mechi za ligi pamoja na barua ya Mosha, ili kamati kujiridhisha na maamuzi hayo," alisema Sendeu.
Alisema kuhusiana na mechi zao za ligi ni lazima wapange mikakati ili kuhakikisha wanashinda mechi zao tatu zilizosalia, ili kujiweka katika mazingira mazuri kimsimamo.
Sendeu alisema kila timu wanayokutana nayo zinakuwa zimewapania kuondoka na pointi tatu, kwa kuwa mzunguko huu ni wa lala salama.
Katika hatua nyingine, viongozi wa matawi ya Yanga jana jioni walitarajiwa kukutana kwa ajili ya kumjadili Mwenyekiti wa matawi Mkoa wa Dar es Salaam, Mohammed Msumi juu ya utendaji wake.
No comments:
Post a Comment