29 March 2011

'Tatizo CCM ni mafisadi, si kukosoa nje ya vikao'

Na John Daniel

VIONGOZI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wametakiwa kujifunza historia ya chama hicho kabla ya kuzungumza na kutambua kuwa kila
mwana CCM wakiwemo viongozi wastaafu au waliopo sasa wana haki ya kuhoji mwenendo wa chama hicho kwa kuwa huo ndio msingi uliojengwa na muasisi wa chama hicho, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Pia viongozi hao wa UVCCM wametakiwa kujihoji kwanza wao kama mali walizonazo ni halali ikilinganishwa na vipato vyao kabla ya kutoa maneno ya kejeli kwa viongozi waastafu na kutambua kuwa kama wamenunuliwa kutumikia kundi fulani, macho ya Watanzania yanayowatazama yatawahukumu hata kabla ya maneno.

Akizungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa jina Dar es Salaam jana, kigogo mmoja wa CCM alisema suala la kujikosoa ni la msingi kwa viongozi waastaafu na waliopo na kwamba Mwalimu Nyerere alipoona badhi ya viongozi wanakwenda kinyume alionya hadharani na kutunga kitabu cha wajisahihishe.

"Ni jambo la kusikitisha na la ajabu sana kuona watu wanakataa katiba, kanuni na utaratibu wa chama, ni sawa na mkiristo kumkemea Mchungaji au padre pale anaposema uzinzi au uasherati ni dambi wakati biblia ndivyo inavyosema.

"Baba wa Taifa aliweka utaratibu wa kutuita mara kwa mara na kutuuliza mambo yanayoendelea kwa wananchi, alipoona baadhi ya watu wanaenda kinyume alitunga kitabu 'cha tujisahihihishe, hakujificha," alisema kiongozi huyo bila kutaka kutajwa jina ili kuepuka malumbano yanayoendelea.

"Inabidi hawa vijana wakajifunze kwanza historia ya chama, hawaijui. Kuonyana ni jambo la kawaida ndani ya CCM na mwazilishi wa utaratibu huo alikuwa Baba wa Taifa mwenyewe.

"Watu wanapewa fedha kununua mitambo ya umeme badala yake wanakodisha mtambo kwa gharama ya juu mara dufu kisha wenye uchungu na nchi hii watulie tu! Haiwezekani, ni kwa nini hao UVCCM wasikemee ufisadi kama wanataka ukweli?," alihoji.

Alisema chanzo cha malumbano yote yanayoendelea ndani ya CCM ni chama hicho kuwakumbatia watu waliochafuka na ufisadi badala ya kuwachukulia hatua ikiwemo kuwaondoa katika nafasi ndani ya chama hicho.

Alisema kwa mujibu wa historia ya chama hicho tangu  enzi za TANU na baadaye CCM, kazi kubwa ya UVCCM ilikuwa ni kukishauri na si chombo cha kukiamulia chama mambo ya kufanya kama inavyofanyika sasa.

"Hao vijana wanatakiwa kujifunza sana, kazi za jumuiya hizi za chama ni kushauri na ushauri wenyewe si hadharani. Matusi wanayotoa kwa viongozi waadilifu wastaafu ndio sasa wanakimaliza chama chetu.

"Huu ndio mfumo mpya ulioanza sasa, ni hatari sana, ni utaratibu mpya ambao haukuwepo na unalenga kuimaliza CCM. Kama watu wanatakiwa wasisema ukweli maana yake ni kuwataka kuwadanganya Watanzania hawa wenye akili kuliko hao vijana, kamwe hatutakubali," alisisitiza.

Alisema mpango wa viongozi wanaofaidika na msimamo wa UVCCM kuwachukuliwa hatua wakosoaji wa chama katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya (NEC) mjini Dodoma mwenzi ujao ndio itakisambaratisha kabisa CCM.

"Kama watathubutu kufanya hivyo maana yake wanataka tuwadanganye Watanzania na hatutafanya hivyo. Sisi tunata wakemee ufisadi na si kutuhamisha kwenye ajenda ya msingi, haya yote chanzo chake ni ufisadi, kama wangeshughulikia mzizi huo haya yote yasingekuwepo," alisema kiongozi huyo.

Habari zilizoifikia Majira kutoka ndani ya CCM zilisema kuwa vikao vya Kamati Kuu (CC) na baadaye NEC vinavyotarajiwa kufanyika Dodoma mwezi ujao vitawaka moto baada ya kundi linaloaminika kuwaunga mkono UVCCM kutaka vigogo wote waliohusika katika kukosoa CCM hadharani wachukuliwe hatua kali.

"Kama viongozi waliohusika katika malumbano wakati wa awamu ya kwanza ya Rais Kikwete hawakuchukuliwa hatua unategemea nini kama si kuendeleza tabia hiyo ya kusemasema nje ya vikao?

Subiri Kamati Kuu na NEC mwezi ujao utaona, watafukuzwa wote waende wanakotaka, baada ya hapo chama kitatulia, maana kuanzia hapo kila mtu ataogopa," kilisema chanzo chetu ndani ya CCM.

Hata hivyo uwezekano wa kuchukua hatua hiyo dhidi ya watu hao ni mdogo kwa kuwa hatua kama hiyo inaweza kukiwepa pabaya zaidi CCM katika uchaguzi Mkuu ujao.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema njia pekee inayoweza kuchukuliwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, ni kukemea watu wanaokwenda kinyume na maadili na miiko ya uongozi na kufumua uongozi wa chama hicho ili kukijenga upya pamoja na kuvunja makundi yote ya urais mwaka 2015, bila kuwaonea haya wenye tuhuma za ufisadi.

Vigogo wanaotajwa kukosoa CCM hadharani bila kuogopa ni mawaziri wakuu wastafu, Jaji Joseph Warioba, Bw. Frederick Sumaye, Bw. Edward Lowassa pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge sasa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samwel Sitta.

Hivi karibuni viongozi wa UVCCM walinukuliwa wakiwashambuliwa viongozi hao bila kuwataja majina, huku wakiwahusisha baadhi yao na mpango wa kusaka urais mwaka 2015, hatua ambayo imeibua malumbano na watu wa mada mbalimbali kujitokeza kuwatetea, na baadhi yao kujitetea.

8 comments:

  1. DU mimi naiogopa ccm, namna inavyo endelea hebu tuone kama tutufika na vile mi naona upinzani ungekua makini ungeweza kutwaha hatamu kwani kule zanzibar washaipunguza makali

    ReplyDelete
  2. CCM kama inataka kuwa mahali salama inatakiwa ihakikishe kuwa ufisadi unakemewa kama baadhi ya viongozi wanavyofanya na kama hawa viongozi wanaokemea ufisadi wataonekana hawafai ndani ya CCM ujue hilo ndiyo litakuwa anguko la chama cha mapinduzi, hivi kwa sasa nani ataweza kukiokoa chama cha mapinduzi mafisadi wapo kila pande ya chama na serikali,ccm iwatimmue wote mafisadi ndiyo itakuwa salama lakini nani anaweza kufanya hayo? tusubiri kikao cha mwezi ujao tuone.

    ReplyDelete
  3. TATIZO LA UVCCM NI UDUNI WA ELIMU DUNIA, HATA UKIONA MANENO WANAYOSEMA NIKAMA VILE MTU HAJAENDA SHULE!NAKAMA WALIMALIZA SHULE BASI WALIMALIZA KWA KUDRA YA MWENYEZI MUNGU MWENYE REHEMA ZOTE.
    KINACHO NISHANGAZA ZAIDI NI KWA NINI MWENYEKITI WA CCM AMEKAA KIMYA NA KURUHUSU HAYA MAJIBIZANO YAKIENDELEA? BILA SHAKA SASA TUNAWEZA KUONA UDHAIFU WA HUYU MWENYEKETI WA TAIFA WA CCM.

    ReplyDelete
  4. yetu macho,tuone km kuna mwenye kumfunga paka kengele

    ReplyDelete
  5. BARUA YA WAZI KWA WANA-CCM.
    Hivi haya maneno na malumbambano ya kila siku hamuoni kuwa badala ya kujenga chama chenu mnakibomoa chama hiki kikongwe? Hivi mwenyekiti wa chama hiki mheshimiwa J.kikwete yuko wapi? hivi kweli anafurahia hali hii ya malumbano yasiyo na tija? hivi mzee makamba kwa hekima ya uzee wake anaona busara kupayuka kila siku kwa mambo yale yale? Sumaye akisema kitu wanamjibu, lakini chadema wakirusha dongo la CCM wanakaa kimya kiasi kwamba wananchi wanafikiri ni kweli yale chadema wanayosema ni kweli! mbona kama katibu wa chama hujibu mapigo ya chadema? mie naona mzee makamba husitahili cheo hicho!ni muda wako mzuri wa kujiuzuru nafasi hii, hapo ulipofikisha chama inatosha!!! unajenge uswahili sana katika chama na sasa umemuambukiza mwenyeketi wa CCM mh. J kikwete uswahili huo.
    Ebu tukumbushane kama siyo mageuzi haya batiri ndani ya CCM ya sasa,enzi ya uwenyekiti wa baba wa taifa hali hii ya kutukanana kada wa CCM kwa kada wa CCM ingeweza kutokea? kwa mtazamo wangu chama cha CCM kimekosa mvuto tena na jinsi kinavyoendeshwa ni ibilisi tu ndiye anayejuwa chama kinatumia dira gani! NINI KINAFANYA KIKWETE KUKAA KIMYA??? bila shaka anahusika na kile kinachoendelea sasa hivi ndani ya chama chake, vinginevyo kikwete ameshindwa kuongoza chama ni bora aachie ngazi kama mwalimu nyerere alivyoachia ili chama hiki kirudiwe na hadhi na heshima kama ilivyokuwa mwanzo.

    ReplyDelete
  6. Tanzania itaendelea kutafunwa na wajanja walioko madarakani hadi hapo watanzania wenyewe watakapo ona sasa ni wakati muafaka wa kuwafuta kazi! kufutwa kwao kazi ni kazi yetu wote sisi watanzania ambao sasa tumechoka na chama kilichoko madarakani ni bora kuwepo na ushinda wa kweli kama Baba wa taifa mwalimu nyerere alisema alipenda kuona CCM inagawanyika kuwa mbili! lakini kwa mtazamo wangu sasa kutakuwa na CCM tatu siku si nyingi, Yaani 1.CCM Uswahili-Mwenyekiti Jakaya Kikwete, katibu Makamba pamoja na wafuasi wake.
    Pia itakuja 2.CCM Mafisadi-mwenyekiti-Edward Lowasa, katibu wake Rostom Aziz na wafuasi wake, mwisho itabaki 3. CCM itikadi- mwenyekiti-pius msekwa, katibu wake joseph Butiku na wafuasi wake! ok kama wewe ni MwanaCCM bila shaka utajuwa wewe jiendae kwenda wapi kama mtaona heri basi jiungeni na chama mbadala na si CCM makundi kwa maendeleo ya nchi.

    ReplyDelete
  7. tumechoka kusikia malumbano yenu nyie CMM! tatizo wote mmeoza! wizi umewajaa ndio maana mnaona mmezidiana ujanja! Ni aheri mpigwe chini ili mjifunze!!

    ReplyDelete
  8. Mzee Sumaye watanzania wanajua kupambanua pumba na ngano. Achana na hao! huenda wenzako wapo kazini!.Wanapotoka kwenye "press" wanapewa bahasha na waliowatuma. Usiumize moyo wako wala usipoteze muda wako!. Sikio la kufa halisikii dawa!. Ukitaka yaishe tangaza kutokugombea 2015! Vinginevyo watanzania watarajie patachimbika!. Hivi kijana mdogo kukukosea heshima kiasi hicho mchana kweupe na hakemewi na viongozi wake wa ngazi za juu!. Yote haya watanzania wanaona! Mimi siyo mwana ccm lakini Kumfanyia jeuri Waziri mkuu mstaafu hadharani ni tusi kwa watanzania wote. Viongozi wasidhani kuwa wanamkomoa Sumaye bali wanakiroga chama tawala mchana kweupe!.

    ReplyDelete