17 March 2011

Taasisi za dini zanyooshewa kidole kwenye kodi

Na Tumaini Makene

IMESHAURIWA kuwa ili serikali iongeze mapato kuinua uchumi wa nchi kutokana na makusanyo yake kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), moja ya
misamaha ya kodi inayopaswa kufutwa ni pamoja na ile inayotolewa kwa taasisi za dini nchini, kwani inatumika visivyo kwa manufaa ya watu binafsi.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Bw. Ali Mohamed Kessy, kuwa taasisi hizo zimekuwa zikitumia kimakosa misamaha hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa bei ghali au kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya watu binafsi.

Bw. Kessy aliyasema hayo jana ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika semina ya wabunge juu ya usimamizi wa bajeti inayoendelea Dar es Salaam, ambapo watendaji wa TRA walikuwa wakiwaslisha mada zao juu ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato nchini.

Itakumbukwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2009/2010, Wizara ya Fedha ilitoa pendekezo la kuondoa misamaha ya kodi kwa mashirika ya umma, kitendo ambacho kiliibua mjadala mkali, kutoka kwa madhehebu yote nchini, ya kikristo na kiislamu.

Viongozi wa dini zote, walimkalia kooni Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, ambaye mapema alikuwa amesema kuwa ufisadi katika baadhi ya taasisi hizo ndio uliofanya serikali ichukue uamuzi huo.

Akitetea hoja ya serikali wakati huo, Bw. Mkulo alisema kuwa baadhi taasisi hizo zimekuwa zikitumia vibaya misamaha hiyo na kwamba alikuwa ameiagiza TRA kutoa orodha ya vitu ambavyo vitasamehewa kodi.

Viongozi wa dini walisema kuwa hoja ya Bw. Mkulo haikuwa na msingi na kwamba angekutana nao kwanza kabla ya kutangaza kufuta misamaha hiyo kwenye bajeti yake ya mwaka 2009/10 aliyokuwa tayari ameisoma, huku wakimtaka kuweka wazi taasisi za dini ambazo zimedanganya katika kupata misamaha ya kodi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya semina hiyo, Bw. Kessy alisema kuwa baadhi ya asasi hizo zimekuwa zikitumia vibaya fursa hiyo ya misamaha ya kodi kwa kutumia mgongo wa dini.

"Tunajua bwana, kule kwetu magari yao akienda mtu anaumwa wanakodisha, yanabeba watu kwa fedha, wanaagiza vitu kwa ajili ya matumizi yao binafsi, tunajua haya mambo, angalia shule za kina (anamtaja), mtoto wa maskini kule hasomi, ada yenyewe mamilioni ya fedha.

"TRA wafuatilie hili, wengine wanaagiza mifuko ya saruji au mabati kisha wanatumia kujenga nyumba zao wenyewe, hii haipaswi, wengine wanafanya biashara hawa, waangiza zaidi ya mahitaji yao," alisema Bw. Kessy.

Akijibu hoja hiyo kwa waandishi, Kamishna wa Forodha wa TRA, Bw. Walid Juma, alisema kuwa pamoja na kuwa mamlaka hiyo inao mfumo wa kufuatilia matumizi ya misamaha hiyo ya taasisi ya dini, bado kuna ugumu katika kutambua matumizi yake.

"Kuna ugumu sana katika kufuatilia kama kweli misamaha hiyo inatumika inavyotakiwa. Udhibiti ni mgumu. Lakini zipo matukio kadhaa ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo. Huko Mbeya wakati
fulani tuliwahi kukamata mabati na saruji ikitumika visivyo ambapo iliyoagizwa ilikuwa haiendani na jengo lenyewe," alisema Bw. Juma.

1 comment:

  1. MISAMAHA YA KODI KWENYE TAASISI ZA DINI ZISIONDOLEWE ILLA KUWE NA UMADHUBUTI WA KUIKAGUWA HIYO MIRADI NA KUIFATILIA,KUWE NA KAMATI MAALUMU YA KURATIBU MATUMIZI YA HIYO MIRADI , MTU ANOMBA MSAMAHA WA SARUJI TANI 1,500 SAWA NA MIFUKO 30,000 UKIFATILIA JENGO LILILOOMBEWA INATUMIKA MIFUKO 500 TUU MINGINE BIASHARA,WAFANYA BIASHARA WENGI HAPA MJINI HUNUNUWA TILES NA VIFAA VYA UJENZI HUKO KURASINI BEI YA JUMLA KITU KIKO WAZI WALA SI KIFICHO WAKATI OMBI NI KUJENGEA MAJENGO YA IBADA NK, LIMULIKWE HILO, MIFANO MINGI SANA HATUKATAI NJIA NYINGI ZA KUJIPATIA VIPATO LAKINI UNAOMBA MSAMAHA KWA AJILI YA HUDUMA ZA HOSPITALI NI SAWA KABISA LAKINI MALIPO UNAYOTOZWA NI SAWA NA HOSPT YA MTU BINAFSI

    ReplyDelete