03 March 2011

AFC yakiri Ligi Kuu ngumu kwao

Na Addolph Bruno

BAADA ya kuchapwa mabao 4-2 na JKT Ruvu juzi, uongozi wa Klabu ya AFC Arusha umekiri kwamba uwezo wao ni mdogo katika Ligi Kuu
Tanzania Bara.

AFC inayoshikilia mkia katika ligi hiyo, ina pointi 11 ambapo imebakiwa na mechi nne dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba, Kagera Sugar na Polisi Tanzania.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya JKT, Mwenyekiti wa AFC Peter Temu alisema baada ya matokeo hayo sasa nguvu zao wanazihamishia katika michezo iliyosalia.

"Kweli hali yetu si nzuri, lakini hii si sababu ya sisi kushindwa kufanya vizuri, ukizingatia tuna michezo minne mpaka sasa, ambayo tutacheza kufa na kupona tushinde," alisema.

Alisema kama watashinda michezo hiyo yote watakuwa wamefikisha pointi 23 kutoka pointi kutoka 11 walizokuwa nazo sasa ambazo zinaweza kuwanusuru na kushuka daraja.

Kuhusu mchezo dhidi ya JKT Ruvu, Mwenyekiti huyo alisema wachezaji wake hawakutulia, ingawa walikuwa na uwezo wa kuibuka na ushindi ambapo hata hivyo mwamuzi wa mchezo huo alikuwa na upungufu wake.

"Siwezi kulisemea sana hilo la mwamuzi, huu ndiyo mpira wa nchi hii ninachoweza kusema mwamuzi hakuwa anatenda haki kwa sababu katika penalti mbili, tumepewa moja na nyingine ikapotezewa," alisema

No comments:

Post a Comment