08 February 2011

Yanga yadaiwa viti Songea

*Yatuma wapepelezi Ethiopia

Na Waandishi Wetu

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU), kimeliandikia barua Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuomba Klabu ya Yanga iwalipe Sh. 230,000 baada ya wachezaji wake kuvunja geti na viti vya Uwanja wa Majimaji katika mechi ya Ligi Kuu iliyofanyika Jumamosi.

FARU imeliandikia shirikisho hilo, baada ya Majimaji kuwaandikia barua ya madai hayo

Wachezaji wa Yanga wamedaiwa kufanya fujo na kuvunja viti 12, pamoja na mlango mmoja katika uwanja huo baada ya mchezo huo, ulimalizika kwa timu hizo kutoka suluhu.

Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Klabu ya Majimaji, Ahmed Dzumba, alisema klabu hiyo imeiandikia FARU barua kuidia Yanga, baada ya kukabwa na hotel ya Majimaji iliyopo mjini Songea kutaka walipwe gharama ya Sh. 180,000 ya viti ambavyo waliazima.

Alisema mbali na viti hivyo pia, klabu hiyo imetakiwa kulipwa sh. 50,000 kama gharama ya geti lililovyunjwa na wachezaji hao lililopo uwanjani hapo.

"Sisi tumesikitishwa sana na vurugu zile, vile viti si vya kwetu tuliazima tu katika ile hotel ili wageni wetu wavitumie lakini sasa tunadaiwa, uongozi wa hotel, umepiga hodi katika ofisi za mkoa kuomba walipwe," alisema Dzumba.

Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umetuma wapelelezi kwenda mjini Addis Ababa, Ethiopia ili kusoma mazingira ya huko na kujihami na hujuma zozote zitakazofanyika.

Timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo wake wa marudiano wa Kombe la Shirikisho (CAF) dhidi ya Dedebits kati ya Februari 11, 12 na 13 mwaka huu, katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, timu hizo zilifungana mabao 4-4.

Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema walishatuma wapelelezi na wameleta taarifa ambazo uongozi umeanza kuzifanyika kazi Sendeu.

Alisema msafara mzima wa timu hiyo unatarajiwa kuondoka nchini Alhamisi, siku moja baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Taifa Stars na Wapalestina.

Sendeu alisema maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yameshakamilika na wachezaji wao wana ari kubwa ya ushindi.Wakati huo huo Sendeu alisema Kocha mpya wa timu hiyo, Sam Timbe na Kaimu Katibu Mkuu Mwesigwa Selestine jana walitambulishwa rasmi kwa wachezaji wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment