08 February 2011

FIFA kuendesha semina ya siku nne

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), linatarajia kuendesha semina ya siku nne nchini kwa Wenyeviti, Makatibu Wakuu na Maofisa Habari wa
Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara itakayohusu mapitio ya awali waliyokubaliana katika Azimio la Bagamoyo.

Azimio hilo lilifanyika Bagamoyo Desemba, 2007 ambapo FIFA ilizitaka klabu hizo kutekeleza na kutafuta ufumbuzi wa muundo wa utawala, mfumo wa idara ya ufundi, vitendea kazi na utawala bora ambapo klabu ziliazimia kutimiza hayo ndani ya miaka mitatu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema semina hiyo itafanyika Februari 14 mpaka 18, mwaka huu jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kupitia waliyokubaliana katika azimio la Bagamoyo.

"FIFA ilikubaliana na klabu yafanyike mapitio ya kile kilichoazimiwa Bagamoyo, baada ya miaka mitatu ili kuona kama utekelezaji wake umefanyika ambapo wenyeviti, makatibu na maofisa habari ndiyo watakaohusika na semina hiyo," alisema Wambura.

Alisema wenyeviti watapata fursa ya kufanya mapitio kwa pamoja na viongozi wengine, ambapo baada ya mapitio hayo viongozi watakaobaki watapata semina kwa siku zitakazofuata.

Wakati huohuo, Wambura alisema Machi 31, mwaka huu kutakuwa na mtihani kwa watakaokuwa wanataka uwakala wa FIFA ambapo mtihani huo, utafanyika jijini siku hiyo kuanzia saa nne asubuhi.

"Tumekuwa tukipata maswali mengi juu ya huo mtihani, sasa kila kitu kimekamilika na utafanyika siku hiyo, hivyo wale waliokuwa wakihitaji sasa ni wakati muafaka kuja kuchukua fomu na kuzijaza," alisema Wambura.

No comments:

Post a Comment