02 February 2011

Mbunge Shinyanga akoleza moto wa Dowans

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MOTO wa kupinga nia ya serikali kutaka kuilipa kampuni feki ya Dowans malipo ya sh. bilioni 94 umezidi kusambaa nchini ambapo mbunge wa jimbo la
Shinyanga mjini (CCM), Bw. Steven Masele ameungana na wananchi wanaopinga kulipwa kwa malipo
hayo.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Shinyanga katika viwanja vya soko kuu mjini Shinyanga juzi, Bw. Masele alisema yeye binafsi anapinga vikali kusudio la serikali kutaka kulipa malipo hayo na kwamba iwapo fedha hizo zitalipwa ni sawa na serikali kuwafanyia dhuluma wananchi wake.

Bw. Masele alisema yeye kama mbunge na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Shinyanga mjini kamwe hawezi kujipendekeza kwa kundi la mafisadi wanaopanga njama za kutaka kuifilisi nchi wakati wananchi wake wakiwa ni masikini wa kutupwa.

Hatua hiyo ya Bw. Masele kuelezea msimamo wake kuhusiana na malipo kwa Dowans ilitokana na wananchi katika mkutano huo kuhoji msimamo wake iwapo anaungana na wananchi kupinga malipo au anaafiki kulipwa kwake kama serikali inavyodai kuwa ni kuheshimu sheria za Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Ndugu zangu wana Shinyanga wenzangu, mimi napenda niwathibitishie wazi kuwa binafsi yangu siko tayari kujipendekeza kwa kundi la mafisadi kwa maslahi binafsi, sikubaliani kabisa na uamuzi wa kulipwa kwa Dowans, ninapata uchungu kulipa matapeli
hao, msimamo wangu ni huo na ninaamini nanyi ndio msimamo wenu, alieleza Bw. Masele.

Alisema pamoja na kushitakiwa katika ICC hukumu iliyotolewa ni ya kuwakandamiza Watanzania nani ni dhuluma kwa taifa changa na maskini kama Tanzania.

Mbunge huyo ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwahutubia wakazi wa mjini Shinyanga tangu alipochaguliwa kuwa mbunge, alishauri serikali iunde
jopo la wanasheria kwa lengo la kukata rufaa na kuepusha nchi kulipa deni hilo kwa matapeli.

"Kuna kila dalili zote zinazoashiria huenda kesi hiyo ilitokana na kupangwa na baadhi ya wajanja wachache na hivyo Dowans kupewa tuzo hiyo bila ya kuzama kwa undan, tutalipaje mabilioni ya shilingi wakati umeme hawakutoa?" alihoji Bw. Masele.

Kuhusu mikataba ya Richmond Bw. Masele alikiri kufanyika kwa makosa na kuisababishia nchi hasara na kwamba sasa inahitajika wahusika kuwajibishwa kutokana na kasoro na dosari katika mikataba iliyofungwa kiujanja ujanja.

8 comments:

  1. Wewe masele acha kuhadaa wewe mwenyewe umebebwa na kutangazwa kwa lazima na hukushinda ubunge wa shinyanga. ulikimbia nini baada ya kutangazwa mshindi pamoja na mkurugenzi wa manispaa kama kweli wewe ni halali? Acha kujikosha kwa mgongo wa richmond na dowans kwetu hatukutaki!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!maana hatujakuchagua bali umechaguliwa na hao DOWANS NA RICHMOND chini ya makamba na ridhiwani,sasa leo unawageuka kweli binadamu hawana fadhila

    ReplyDelete
  2. ni kichefuchefu kwa maselle kuongea masuala hayo coz uliona wapi ktk historia ya Tanzania mbunge anashinda kwa kura moja?????????
    tafadhali nyamaza kabisaaaaaaa.

    ReplyDelete
  3. Bw. Steven Masele huwezi kukata mkono unaokulisha, labda uwe taahila. Dowans ina uhusiano wa karibu sana na CCM kilichokuingiza kwenye ubunge, pesa za mafisadi ni sehemu ya ushindi wako wa ubunge. kupinga dowans kulipwa ni kupinga CCM kuwepo madalakani. Usidsnganye wananchi wako kwa kuimba wimbo wao wa kupinga dowans na kutaka katiba mpya. Kama uko serious kweli hama 'huko' uliko nenda 'kuleee' waliko wapinga dowans wa kweli

    ReplyDelete
  4. kama wananchi wenye nchi hawataki kuilipa dowans wasilazimishwe kulipa na mwananchi mwenzao ama kikundi cha watu. Ngoja tusubili hatua zitakazochukuliwa na dowans kwa kutokulipwa na watanzania, tuko tayari kwa matokeo hayo kama nchi lakini CCM isitulazimishe, tusipoteze muda wetu kujadili mafisadi, sasa tujadili vitu vingine kama matokeo mabaya kwenye shule za kata ikiwezekana pesa ambazo dowans inataka ilipwe tuzielekeze kwenye shule za kata ili ziwe na ahueni

    ReplyDelete
  5. Tolerance, tolerance, tolerance Ndugu zangu. Masele ni Mbunge kama alivyo Rais wetu. Iwe isiwe hivi sasa wao ndio wawakilishi wetu. Yeye ametoa dukuduku lake. Acheni akose fadhila. ila aegemee upande wenu. Si kondoo aliyepotea amejirudi. hata kwa mara hii amewapa tafu. Tuwe na subira. Si kila kingaacho ni dhahabu. Hata huko upinzani yapo madudu, kama mungejua. Kwa hiyo Mhe. Masele ana haki ya kutoa dukuduku lake na kusikilizwa. Alichosema ni kweli na kama wana CCM wote wangechukuwa msimamo huo tungepiga hatua. Huyu ni SHibuda mwingine, msubirini. Days will tell.

    ReplyDelete
  6. NAWE SULEMAIN ABED ACHA NJAA KUSIFIA VITU AMBAVYO HAVIPO WOTE TULIKUWA KWENYE UWANJA HUO MAELFU YA WATU YAMETOKA WAPI HII HABARI UMEITENGENEZA BAADA YA KUPATA MAELEKEZO KUTOKA KWA RC BALELE AMBAYE HUWEZI KUANDIKA HABARI HADI UMUULIZE HIVI UNAANDIKIA MAJIRA AU BALELE NEWS PAPER MBONA ALIPOSHUSHULIWA NA SHIBUDA KWENYE KIKAO CHA RCC HUKUANDIKA HUYO SI MBUNGE WA SHINYANGA WEWE MWENYEWE ULIANDIKA ALIVYOTANGAZWA KINYEMELA NA KESI ATASHINDWA KUWENI WAANDISHI WASTAARABU,SISI WASOMAJI TUNAWAELEWA SANA WAANDISHI WA SHINYANGA KILA MTU NA MTU WAKE WEWE NI WA BALELE.MBUNGE WETU NI SHELEMBI.ACHA UNAFIKI ABED.

    ReplyDelete
  7. Hizo pesa mnazotaka kuilipa dowans (ambao ni mafisadi watanzania waliojificha chini ya kivuli cha dowans) si mngeweka maabara kwenye shule zenu za kata mlizozianzisha ambazo zimefelisha kuliko maelezo, na vitabu kwa ajili ya shule hizo pia mngeweza kuzitumia hizo pesa kwa ajili ya kuweka sawa mashirika mawili ya usafiri la kwanza ATC muiwezeshe kupata ndege za kutosha na pili RELI YA KATI au mnasubiri kusukumwa na NGUVU YA UMMA KAMA TUNISIA?

    ReplyDelete
  8. ccm someni nyakati,kuilipa dowans ni kuiangusha ccm,2015,katiba mpya tume huru ya uchaguzi hamfiki popote nyie

    ReplyDelete