23 February 2011

Wabunge wafungua kesi kupinga Dowans

*Wananchi wengine waunga mkono

Na John Daniel

KATIKA hali inayodhihirisha Watanzania kukerwa na malipo ya Kampuni ya Dowans, Mahakama Kuu ya Tanzania imepokea na
kusajili kesi ya kikatiba kupinga malipo hayo.

Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa mahakamani hapo jana na Watanzania saba wakiwemo wabunge watatu na kupewa namba tano ya mwaka 2011 chini ya Kampuni ya Mawakili ya Mpoki na Lukwaro.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, msingi wa kesi hiyo ni kwamba malipo ya Dowans ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sehemu ya tatu kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili.

Katika kesi hiyo Watanzania hao wanaiomba Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa malipo hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na katiba ya nchi.

"Sisi kama Watanzania wenye uchungu na nchi yetu, tunahurumia taifa letu na watu wake masikini wanaokosa hata huduma muhimu kutokana na hali ngumu, tumeamua kwenda kuomba haki Mahakama Kuu," alisema Bw. Senkoro Nzoka mmoja wa Watanzania hao.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili malipo ya Dowans ni uvunjaji mkubwa wa katiba ya nchi kwa kuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi.

"Kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili inataka kila mwananchi kulinda rasilimali za nchi, sisi kama Watanzania tuna wajibu kuhakikisha rasilimali za nchi hazichezewi," alisema Bw. Senkoro.

Kifungu hicho cha Katiba kinasomeka- "27.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, Kulinda mali ya umma, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao," inasema sehemu hiyo ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Alisema kifungu hicho ndio msingi wao wa kufikia maamuzi ya kufungua kesi hiyo wakiwawakilisha Watanzania.

Hata hivyo Bw. Nzoka alisema hawezi kutoa ufafanuzi wa kina juu ya kesi hiyo kwa kuwa ni suala la kisheria na kuweka wazi kuwa anachoweza kukiri ni kwamba wamejitolea kuwawakilisha wanannchi wasio na uwezo watakaoathirika kukosa huduma muhimu.

"Kama unavyojua hili ni suala la kisheria kwa sasa, siwezi kusema zaidi lakini tambua kuwa wabunge wa CCM walikataa na kuitaka serikali kutafuta njia ya kuepusha malipo hayo, huo ndio mwongozo wetu," alisema Bw. Nzoka bila kutoa ufafanuzi wa kina.

Uchunguzi wa Majira ulibaini wabunge watatu wanaowakilisha wenzao katika kesi hiyo kuwa ni Mbunge wa Kibakwe, Bw. George Simbachawene, Bi. Anjela Kairuki pamoja na Bw. Gosbert Blandes.

Naye Bw. Hassan Nassoro ambaye ni kijana msomi Mtanzania aliyekuwa nchini Uingereza alisema atazungumzia kesi hiyo baadaye kwa kuwa ni suala la kisheria huku akithibitisha kuwa yeye ni mmoja kati ya walioifungua.

Sakata la malipo kwa Kampuni ya Dowans limekuwa kero kubwa kwa Watanzania tangu ilipoibuka kupitia vyombo vya habari na bungeni.

Awali ilidaiwa kuwa malipo hayo yalikuwa ni bilioni 195 lakini baadaye ilibainika kuwa taarifa hizo zilipikwa na watu wenye manufaa na kampuni hiyo kwa lengo la kuwaibia Watanzania.

Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa kuwa ni uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara ICC) malipo hayo ni sh. bilioni 94.

Katika hatua inayoonyesha suala hilo kukumbwa na giza nene juzi mtu aliyedai kuwa mmiliki wa kampuni hiyo alitingwa nchini na kuzungumza na wahariri wa vyombo vya habari kwa masharti ya kutopigwa picha.

Sharti hilo limezua utata mzito huku Watanzania wengi wakidai kuwa mtu huyo si mmiliki wa kampuni hiyo na kuwa uenda amenunuliwa na wahusika ili wafikie lengo lao la kuvuna jasho la Watanzania la sh. bilioni 94.

Hii ni kesi ya pili kupinga malipo ya Dowans, kesi ya kwanza ilishafunguliwa na asasi za kiraia zipato 50 zikiwakilishwa na Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC).

11 comments:

  1. Nyie wabunge wa ccm acheni kujikosha na kuturubuni watanzania, je nyie mna uwezo wa kumfunga raisi wenu pamoja na mhasibu wenu wa chama? mbona hamuwafungulii wamiliki wa RICHMOND na DOWANS kwa kuvunja katiba kwa kutumia vipengele vya uhujumu uchumi? tungesikia mnawafungulia mashitaka rostam na lowasa pamoja na baba yenu tungesema jambo lakini kipengele hicho cha katiba mnachotumia hakina masilahi hata kidogo kwani kinawaacha wezi wa nchi badala yake unakinga usimlipe mwizi ambae tayari alishaiiba!!!!!!!!!!!!!!!!!huu ni ushenzi mtupuuu..........................

    ReplyDelete
  2. Wewe Anonymous, yaani akili zako ni duni kiasi kwamba hao hao viongozi wa ccm wamewekwa madarakani na hela za Dowans, EPA na nynginezo? Uko wapi wewe au umepofushwa na hao mafisadi. Hujui hata vyama tawala na mafisadi wao kule Tunisia na Misri yaliyowapata. Hawakujua kamwe kwamba nguvu ya wananchi ingewangoa. Wako wapi sasa. Au unadhani CCM yako hiyo ina tofauti?

    ReplyDelete
  3. Wabunge wa CCM scheni unsfiki wenu! Hii kesi yenu labda mnataka kujiosha tu au ni changa la macho kama ile kesi ya TANESCO ili mkishindwa mseme kama Ngeleja tumeshindwa tukubali yaishe!
    Unafiki wenu unakuja pale mafisadi kama Rostam, Chenge, Lowassa mnawarundikia madaraka! Hivi juzi tu mmeliabisha taifa kumfanya Edward Lowassa mwenyekiti wa Tume ya Bunge ya Ulinzi, mambo ya nje! Kama vili hamjui Lowassa ndio DOWANS!

    ReplyDelete
  4. CCM ni Dowans, inafahamika kuwa Dowans ina uhusiano wa nafasi za Makinda, J. Makamba na Lowassa bungeni. Tusipoteze muda na pesa kujadili Dowans, tuchukue hatua ngumu na pengine chungu kwetu kuweka mbambo sawa. Mgawo wa umeme ni wa makusudi ili kulainisha nyoyo za wananchi wakubali mitambo ya Dowans iwashwe. CCM oyee!!

    ReplyDelete
  5. Blendes kama yumo ndani inashangaza! Si mbunge halali wa Karagwe, si ndiye aliyechakachua matokeo na yakatangazwa chini ya ulinzi wa mabosi. AJABU NA KWELI

    ReplyDelete
  6. Kweli nimeamini siku hizi kwa CCM uongozi ni kutafuta ulaji(biashara).Yaani mtuhumiwa wa uhujumu uchumi na madowans anaenda ikulu kuongea na rais wa nchi? Hii kali kweli kweli!

    nawashauri hawa wabunge wa CCM wanaoipinga Dowans mahakamani, wapigie kwanza kura ya kutokumuamini rais kwa kumkaribisha mmliki wa dowans ikulu.

    ReplyDelete
  7. Mimi naomba kila Mtanzania mwenye ushahidi wowote juu ufisadi sio wa Dowans pekee, uwe wa serikali au mwengineo tafadhali hifadhi ushahidi huo kwani ipo siku haki na ukeli vitadhihiri. ambapo mwishowe rasili mali ya nchi zitarudishwa kwa wenyewe pamoja na faida, na kushudia wasiotarajiwa wanakwenda gerezani.

    ReplyDelete
  8. Asante watanzania ambao mmetambua kuwa wabunge wa ccm ni waongo wanataka kutulaghai tu. Wao waanze kumkataa Rostam ambaye ni mhasibu mkuu wa ccm, pia Lowasa ambaye kapewa madarka ktk kamati za Bunge wakati aliwajibika kwa kesi ya wizi wa fedha za taifa hili; bado Kikwete mwenyekiti wenu wa chama amenyakua madaraka. Muwashtaki hao kwanza ndio tutaona kweli mnania njema vingenevyo ni usanii mtupu.Serikali ya ccm inapaswa kuondolewa madarakani maana imeshindwa na inawabeba mafisadi na kuwalinda kila kukicha. Watantania jambo moja la msingi tufanye kama Tunisia , Misri na sasa Libya, kama tunakerwa kweli na hali ya wachache kuifaidi nchi hii.

    ReplyDelete
  9. mambo yanayolizunguka suala la umeme ni moja ya uhalifu dhidi ya binaadamu ambao unatekelezwa na watu wachache walioamua kushirikiana kupora kodi za wananchi.
    Mambo haya na mengine kama haya yanahatarisha usalama wa Taifa. Enzi za mwalimu upuuzi huu usingevumilika.

    ReplyDelete
  10. AISEEE hii ni kweli? yaani hawa wabunge CCM wanataka kutufanya sisi watanzania hamnazo? Wamechelewa! Lowasa, Rostam, Karamagi, Msabaha, Ngeleja, Chenge, Meghji, Masha, Husein Mwinyi, Hossea, Mwakapugi, Mwanyika, Mrindoko na wengi wengineo. Mmeshindwa kuwawajibisha leo mnajifanya kwenda Mahakamani! Kwendeni zenu, hamna maana.

    ReplyDelete
  11. Hawa wabunge vipi? Wanafikiri wananchi wanafikiri kwa tumbo badala ya akili kama wao? Hebu waache upuuzi wao! Tena wasirudie kujaribu kuudanganya umma, kwani wanajidanganya wenyewe.

    Wananchi, tuweke mgumu hadi kieleweke. NIna imani kinachotakiwa kwa sasa ni mtu wa kuongoza tu, na wooooooote watafuata hadi Ikulu kumtoa nduli pangoni.

    ReplyDelete