23 February 2011

TANESCO tayari kuzungumza na Dowans

Na Grace Michael

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema liko tayari kukutana na mmliki wa mitambo ya Dowans kwa ajili ya mazungumzo ili kuinusuru
nchi na janga la mgawo wa umeme ambalo linatishia kuporomoka kwa uchumi.

Hatua hiyo ilifikiwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw. William Mhando wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao walitaka kujua kama shirika hilo limeshakutana na mmiliki wa mitambo hiyo au kama mitambo hiyo imeshawashwa.

Sisi hatujakutana na huyo mmiliki wa mitambo na wala hiyo mitambo hatujaiwasha...kumbukeni hili suala ni la kisheria na sisi tusingependa kuvunja sheria zilizopo lakini kama atakuja kwa ajili ya mazungumzo tuko tayari kuzungumza naye kwani lengo ni kuinusuru nchi na janga hili ambalo sasa linatishia kupomoa uchumi wetu, alisema Bw. Mhando.

Hata hivyo, Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, Bw. January Makamba ilithibitisha kuwa TANESCO imepokea barua ya mwaliko wa mazungumzo kutoka kwa mmiliki huyo.

Kutokana na hatua hiyo, Bw. Makamba alisema kuwa wao kama kamati wangesisitiza TANESCO kufanya mazungumzo na mmliki huyo wa Dowans ili kupunguza tatizo la umeme ambalo linaikabili nchi kwa sasa.

Unajua hata jana (juzi) tulikutana na wamiliki wa viwanda nao walisema namna tatizo la umeme linavyokwamisha kazi zao na linavyotishia ajira za wananchi, hivyo kama kuna uwezekano wa hiyo mitambo kusaidia basi wafanye mazungumzo ili kunusuru hiyo hali, alisema Bw. Makamba.

Akitoa taarifa ya kilichozungumziwa na kamati hiyo, alisema kuwa mjadala mkubwa ulijikita katika suala la umeme pamoja na mafuta ambapo wengi walihoji kuwepo kwa mfumuko wa mafuta na ubora wake.

Aidha alisema kuwa kamati iliweka msisitizo kwa wizara kuharakisha upatikanaji wa umeme ili tatizo hilo limalizike kwa kuwa limekuwa kero kubwa kwa nchi.

Kwa kweli kamati inachotaka ni umeme kuwaka...tumechoka na mipango ya kila siku...na kama mipango hiyo inachelewa kwa urasimu basi ishughulikiwe haraka ili lengo lifikiwe, tunajua kuna mpango wa kukodisha majenereta, mradi wa Dar es Salaam na Mwanza wenye jumla ya megawati 160 hivyo michakato hiyo ifanywe haraka ili miradi hiyo ikamilike, alisema Bw. Makamba.

Kwa upande wa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja alipohojiwa kuhusu kuwashwa kwa mitambo ya Dowans alisema hana jibu la suala hilo kwa kuwa liko mahakamani hivyo hawezi kulizungumzia.

Kamati ya Nishati na Madini leo itatembelea TANESCO kwa ajili ya kuona mambo mbalimbali yanayofanywa na shirika hilo.

3 comments:

  1. Tanesco tumieni taaluma yenu kumaliza tatizo la umeme. Achaneni na wabunge wanaotafuta umaarufu kupitia tatizo la umeme, mawazo ya mh January yanapaswa kufanyiwa kazi haraka kunusuru taifa. Kuna baadhi ya wanasiasa hawapendi tatizo la umeme liishe kwani hilo ndio jukwaa lao la kupatia umaarufu kwani huwa hawana jipya la kuwafanya waonekane

    ReplyDelete
  2. mmmmmm! Dowans ndio njia pekee ya kuondoa matatizo ya umeme???

    Kama ndio hivyo hii kampuni haina mbele wala nyuma!

    ReplyDelete
  3. Tusidanganyane hapa!! Bora tuseme ukweli!! Siasa ni Biashara na biashara ni Siasa za TZ.
    Uwongo, ulaghai vinazidi kwa mbali UKWELI...
    Inabidi tukubali...

    ReplyDelete