Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limekiandikia Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), kuteua Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya
vijana chini ya umri wa miaka 23 (Vijana Stars) kwa ajili ya michuano ya Olimpiki.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 27, mwakani na kumalizika Agosti 12 katika jiji la London nchini Uingereza ambapo michezo mbalimbali itakuwepo kwenye michuano hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Vijana Stars itaanza kampeni zake za kuwania kucheza michuano hiyo Machi 26, mwaka huu kwa kuumana na Kameroon ugenini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura ilieleza kwamba kocha atakayeteuliwa na ZFA, atapaswa kuchagua wachezaji kati ya 10 mpaka 15.
"Baada ya kufanya uteuzi huo, wachezaji hao watajiunga moja kwa moja na wenzao 25, ambao wameanza mazoezi leo (jana) chini ya makocha Addolph Richard na Jamhuri Kihwelo," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema baada ya wachezaji hao kutoka Zanzibar kuungana na wenzao kwa ajili ya mazoezi, benchi la ufundi litafanya mchujo ili kubaki na kikosi cha mwisho cha wachezaji 25, ambacho ndicho kitakachoikabili Kameroon.
Aliongeza kwamba Vijana Stars inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki kati ya Machi 12 au 13 na 19 au 20 mwaka huu. Safari ya Yaounde kwa timu hiyo inatarajiwa kufanyika Machi 22 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment