Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF), katika uchaguzi uliofanyika leo jijini Khartoum, Sudan.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura ilisema Tenga aliyekuwa akigombea kupitia Kanda ya Mashariki na Kati, alimshinda Celestine Musabiyima wa Rwanda, aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.
Tenga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), alipata kura 34 dhidi ya 19 za mpinzani wake.
Rais huyo wa TFF, anakuwa Mtanzania wa pili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF, baada ya Said Hamad El Maamry, ambaye aliwahi kushinda nafasi hiyo mwanzoni mwa miaka ya 80, kwa vipindi viwili mfululizo.
Alishindwa kutetea nafasi hiyo katika kipindi cha tatu, baada ya TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu (FAT), kutoidhinisha jina lake CAF.
El Maamry hivi sasa ni mjumbe wa heshima wa CAF.Mtanzania mwingine aliyewahi kuwania nafasi hiyo mara mbili, lakini hakufanikiwa kushinda ni Muhidin Ndolanga, ambaye aliwania wakati huo akiwa Mwenyekiti wa FAT.
Kalusha Bwalya naye amefanikiwa kwa mara ya kwanza kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya CAF, baada ya kuchaguliwa akiwakilisha Kanda ya Kusini mwa Afrika.
Nafasi ya Kanda ya Magharibi mwa Afrika, ilikwenda kwa Kwesi Nyantakyi wa Ghana.
No comments:
Post a Comment