Na Addolph Bruno
SIKU moja baada ya kuanza mazoezi kujiandaa na michuano ya kufuzu kucheza fainali za Olimpiki, Kocha Mkuu wa timu ya vijana chini ya umri wa
miaka 23 'Vijana Stars' Jamhuri Kihwelu 'Julio' amesema hana wasiwasi na uwezo wa wachezaji aliowachagua.
Ngorongoro Heroes ilianza mazoezi ya nje ya kambi jana, kujiandaa na mashindano hayo ambapo itaanza kampeni zake dhidi ya Cameroon Machi 26, mwaka huu nchini humo kwa ajili ya fainali zitakazofanyika mwakani London, Uingereza.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Julio alisema wachezaji wake wameanza mazoezi wakiwa na ari nzuri, licha ya kuwa siku moja bado haimtoshi kukitambua vyema kikosi chake.
"Mambo yameanza vizuri kabisa, wachezaji wangu ni waelewa kama nilivyosema jana (juzi), ingawa leo ni siku ya kwanza nadhani nitakuwa na wakati mzuri wa kukifahamu vyema kikosi baada ya siku mbili, tatu hivi," alisema Julio.
Alisema ameongeza wachezaji wengi wazoefu ambao wengine wanashiriki Ligi Kuu na Ligi Daraja la kwanza, kabla ya kuchaguliwa kutengeneza kikosi hicho, hivyo hana wasiwasi nao.
Aidha Julio alisema kutokana na hali halisi ya muda kuwa mfupi, leo wanaanza kufanya mazoezi mara mbili kwa maana ya asubuhi na jioni baada ya kufanya mara moja jana, ili kuutumia vizuri muda ambao wamebakiwa nao.
Julio alisema baada ya mazoezi ya uwanjani wanatarajia pia kutenga muda kufanya mazoezi siku saba mchangani, ili kujenga stamina kwa wachezaji wake kabla ya kukutana na Cameroon.
No comments:
Post a Comment