23 February 2011

Misaada ya mikate, biskuti yapingwa Gongolamboto

Na Gladness Mboma

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Sadick amewaomba wahisani wanaopeleka misaada kwa ajili ya waathirika wa milipuko ya
mabomu Gongolamboto kutoa vyakula vinavyokidhi haja zao na siyo kutoa mikate na biskuti pekee.

Hayo yalisemwa na jana Dar es Salaam jana, Bw. Sadick wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya makusanyo ya vyakula vya misaada.

"Tunashukuru kampuni, mashirika na wasamaria wengine wameendelea kutoa misaada kwa hali na mali, lakini misaada hiyo mingi imekuwa ni mikate na biskuti," alisema.

Alisema kuwa kwa sasa wananchi wanahitaji misaada ya vyakula kama  maharage, sukari, michele, unga, mahindi na vitu vingine kama malazi.

Bw. Sadick alisema kuwa wanashukuru kwamba mpaka sasa serikali haijaanza kutoa msaada wa chakula na kwamba misaada mingi imetoka kwa wasamaria wema.

Alisema kuwa awali wakati walipokuwa wakitangaza kuomba misaada waliorodhesha misaada ambayo inahitajika, lakini anashangaa kuona watu wakiendelea kupeleka mikate na biskuti kwa wingi.

Naye mmoja wa wasimamizi wa misaada hiyo ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa siyo msemaji alisema kuwa wanaogopa kupeleka misaada hiyo ya biskuti kwa waathirika hao kwa kuofia kutukanwa.

"Unajua hawa waathirika ukiwapelekea biskuti hawatatuelewa hata kidogo tnapeleka kwanza vyakula kama vile sukari, maharage, unga na mchele na baadaye tutaanza kuwasambazi hizi biskuti,"alisema.

Alisema kuwa kama mikate inaharibika mara moja na mingine inafika ikiwa imevunda na kuwataka watu walioamua kujitolea kutoa misaada hiyo watoe vyakula vya kudumu.

Majira ambayo ilifika katika eneo la shule ya sekondari ya Pugu kunakohifadhiwa vyakula hivyo vya misaada ilishuhudia chumba kimoja kikiwa kimejaa mikate, pipi na biskuti na huku mingine ikiendelea kupelekwa.

Wakati huo huo Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Edward Lowassa imetembele waathirika wa mabomu, ambapo waathirika hao waliiomba kamati hiyo kuieleza serikali juu ya kuharakisha tathmini ya majengo na mali zilizoaribika.

Bw. Lowassa aliwataka waathirika hao kuondoa wasiwasi na kwamba ombi lao watalipeleka katika Kamati inayoshughulikia maafa hiyo ili tathmini iweze kufanyika haraka.

Naye Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Bw. Shamsi Vuai Naodha ambaye alitembelea waathirika hao wa mabomu alisema kuwa amekwenda kuangali kama kuna upingufu wa vitu na ulinzi ikiwa ni pamoja na kungalia tathmini itakuwaje.

Wakati huo huo kampuni mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi na wasamaria wema wameendelea kumiminika kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao.

Kampuni ya bima Dar es Salaam imetoa msaada wa mahindi, maharage, unga na maji vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 5.

Meneja wa Masoko wa Kampuni hiyo ya bima, Bw. Amani Boma alisema kuwa wamesikitishwa na janga hilo ambalo limetoa uhai wa wananchi na kusababisha maafa.

3 comments:

  1. Wee mkuu wa mkoa vipi? kwani mkate na biscuit si vyakula. Kama mtu uwezo wake ndio huo kwanini asichangie vyakula hivyo? Wakati mwingine nyie wanasiasa mnanipa kichefuchefu.
    Watu watoe kwa uwezo wao, mradi tu wasitoe vyakula vibovu. Wee unaacha kuwaambia mafisadi wachangie angalau kutokana na hela yaliyotuibia unabaki kuongea upuuzi wa kupinga michango ya mikate na biscuit! Una jipya?

    ReplyDelete
  2. WE MKUU WA MKOA UMETOA NINI?ZAIDI UNASUBIRI POSHO ZA VIKAO KUHUSU HIYO GHARIKA.

    ReplyDelete
  3. NYIE VIONGOZI WA CCM WANAFIKI WAKUBWA UMEMUONA MAKINDA ETI ANALIA NA KUJIFANYA MWENYE UCHUNGU, UONGO MTUPU HAKUNA KITU PALE MNAFIKI TU EUMESHA JUA NJAMA ZAO, WANAFIKI NYIE WAACHENI WNO WEZA KUPELEKA HATA BISCUTI WAPELEKE. UONGOZI WENU MBAYA NDIYO SUMU YA WATANZNIA KWA SASA MPAKA MTUMALIZE

    ReplyDelete