23 February 2011

Kesi ya ufisadi wa elimu yahairishwa

Na Rehema Mohamed

MDAIWA katika kesi ya madai iliyofunguliwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga dhidi ya Mwanaharakati Bw.Kainerugaba Msemakweli ameiomba
mahakama ya Wilaya ya Ilala kutupilia mbali kesi hiyo kutokana na mdai kutoudhuria mahakamani kesi inapopangwa kusikilizwa.

Bw. Msemakweli alitoa ombi hilo jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu, Bi. Esther Mwakalinga wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa.

Bw. Msemakweli alidai kuwa mahakama ina wajibu wa kuchukua hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu kidogo cha sheria namba 9(8) cha kesi za madai kama kinavyosema kuwa kama mdai hatokei mahakamani bila ya kutoa taarifa, mahakama inapaswa kuifuta kesi hiyo.

"Kutohudhuria kwake mahakamani ni sawa na kutupotezea muda sisi wengine tena wakati mwingine hatoi sababu ya kufanya hivyo, naomba mahakama itupilie mbali madai yake kama sheria inavyosema," alisema Bw. Msemakweli.

Aliongeza kuwa kama yeye asingehudhuria, sheria ingemhukumu na kuongeza kuwa hivyo hivyo mahakama ichukue hatua za kisheria dhidi ya mdai.

Kutokana na maelezo hayo, Bi. Mwakalinga alisema kuwa mahakama itazingatia malalamiko ya mdaiwa kama alivyoyawasilisha mahakamani.

Aliongeza kuwa mahakama hiyo ingetoa hairisho la mwisho la kesi hiyo hadi Machi 21 na kama Dkt. Mahanga hatoudhuria, mahakama itachu hatua.

Katika kesi hiyo Dkt. Mahanga anamdai Bw. Msemakweli sh. bilioni moja kutokana na kumtaja kwenye orodha ya mafisadi wa elimu.

Mbali na kudaiwa kughushi vyeti vya elimu pia Dkt. Mahanga anadaiwa kuchukua fedha za umma kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuzitumia kwa ufisadi.

No comments:

Post a Comment