08 February 2011

Lengo si kufukuza machinga wa Kichina-Dkt. Chami

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema operesheni inayoendelea sokoni Kariakoo imelenga kukagua na kubaini wafanyabiashara wote wanaofanya
biashara kinyume cha leseni zao tofauti na madai kwamba imelenga kuondoa wamachinga wa Kichina.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami alipoombwa na gazeti hili kwa njia ya simu kutoa ufafanuzi kuhusu operesheni hiyo.

Akizungumza kutoka mjini Dodoma anakohudhuria mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dkt. Chami alisema operesheni inayoendelea, inawahusu wafanyabiashara wote wanaofanya biashara eneo hilo kinyume cha leseni zao na haiwalengi watu wa aina moja.

"Kinachofanyika Karikakoo ni operesheni ya kubaini wale wote wanaofanya biashara kinyume na leseni zao. Kama mtu aliomba leseni ya wholesale (kuuza jumla), badala yake anafanya retail (kuuza reja reja) huyo ndiye tunamtafuta," alisema Dkt. Chami na kuongeza;

"Operesheni hii hailengi kundi la watu, kama baadhi wanavyoda, inahusu wafanyabiashara wote awe mtanzania au yeyote yule. Kama mtu aliomba kibali cha kujenga kiwanda, akazalisha bidhaa za kutosha, halafu akaomba kibali na kufungua biashara ya rejareja kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazokubalika, huyu hana makosa."

"Hatuna ugomvi na raia yeyote, awe wa kigeni au Mtazania ili mradi anafuata sheria na taratibu zilizowekwa katika kufanya biashara yake. Operesheni hii si ya kufukuza Wachina bali ni kusaka wanaofanya biashara kinyume cha leseni zao. Hatuko hapa kuwafukuza watu wa taifa fulani.Tunasaka wale wanaofanya biashara kinyume cha leseni walizoomba, halafu  tutajua namna ya kuwaelimisha ili wafanyebiashara zenye tija kwao na uchumi wa taifa kwa ujumla."

Hivi karibuni wizara hiyo kupitia naibu Waziri wake Bw. Lazaro Nyalandu ilikaririwa ikitoa siku 30 kutaka wafanyabiashara wote raia wa China wanaofanya biashara za kimachinga sokoni hapo, kuondoa.

Bw. Nyalandu alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla sokoni hapo akiandamana na viongozi wa Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam ambapo aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha kuwa wanaondoka sokoni hapo kabla ya muda huo.

1 comment:

  1. Unafiki mkubwa viongozi wa nchi hii, mara machinga wa kichina waondoke, mara hatuna ugomvi nao! hamfahamiki

    ReplyDelete