24 February 2011

Kina Kikwete wakutana na vurugu Ivory Coast

Na Mwandishi Maalumu

WAKATI vurugu zililipuka juzi mitaani nchini Ivory Coast kushinikiza kiongozi aliyeng'ang'ania madarakani, Bw. Laurent Gbagbo aachie ngazi, Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wenzake wa Afrika wanaotafuta ufumbuzi wa mzozo wa kisiasa katika nchi ya Afrika Magharibi ya Ivory Coast juzi walikutana kwa zaidi ya saa tatu na mmoja wa mahasimu hao waliojitangaza marais wa nchi hiyo.

Katika jiji la Abidjan, wafuasi wa Bw. Alassane Ouattara aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi kama mshindi waliingia mitaani kupinga mpinzani wake, kitendo kilichosababisha vifo vya askari watatu.

Wanajeshi wanaomuunga mkono Bw. Gbagbo walisema wamechokozwa kwa kuwa wafuasi wa Bw. Ouattara walikuwa na silaha, hivyo tangu asubuhi kulikuwa na kurushiana risasi na wananchi waliojazana mitaani.

Rais Kikwete na viongozi hao wa nchi za Mauritania, Chad na Afrika Kusini walikutana na kufanya mazungumzo na Bw. Gbagbo, mmoja wa wanasiasa ambao wamejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Novemba 28, mwaka jana.

Kwa muda mwingi wa mkutano huo katika Ikulu ya Ivory Coast mjini Abidjan, viongozi hao walimsikiliza Bw. Gbagbo na kumuuliza maswali katika hatua hiyo ya kwanza ya kazi ya ujumbe wa viongozi hao ambao ni kuwasililiza na kuwauliza maswali wadau wote katika mzozo huo, ambao umeiacha Ivory Coast ikiwa na marais wawili, serikali mbili na uwezekano mkubwa kuwapo makundi mawili ya watu wenye silaha na waliko tayari kuzitumia kuwania madaraka ya kuongoza nchi hiyo.

Katika mkutano huo, Bw. Gbagbo alidai kuwa yeye ndiye Rais halali wa Ivory Coast kwa sababu alishinda raundi ya pili ya upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana nchini humo.

Viongozi hao wako Ivory Coast kutekeleza azimio la Umoja wa Afrika (AU) ambao katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za AU mwezi uliopita mjini Addis Ababa, Ethiopia, uliteua kundi la nchi sita za Afrika chini ya uenyekiti wa nchi ya Mauritania kutafuta suluhisho la amani katika Ivory Coast.

Nchi zinazounda kundi hilo chini ya uenyekiti wa Mauritania ni Tanzania, Afrika Kusini, Chad, Burkina Faso, Equatorial Guinea ambayo ndiyo mwenyekiti wa sasa wa AU pamoja na Nigeria ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Nchi hizo zilifanya kikao cha kwanza Jumapili ya wiki hii mjini Nouakchott, Mauritania kabla ya kusafiri kwa kuja mjini Abidjan kukutana na pande zote zinazovutana katika mzozo huo wa kisiasa wa nchi hiyo ya Ivory Coast.

Kutwa nzima ya jana, viongozi hao walikuwa wamepanga kukutana na makundi ya watu na taasisi mbalimbali za wadau wa suala hilo la Ivory Coast.

Miongoni mwa watakaokutana na marais hao leo ni pamoja na Bw. Alassane Quattara, ambaye kama alivyo Gbagbo, amejitangaza kuwa Rais wa Ivory Coast kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu huo wa mwaka jana na pia naye ameunda serikali yake.

Makundi mengine yanayokutana na viongozi hao leo ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Ivory Coast, Bw. Choi; wajumbe wa Baraza la Katiba la Ivory Coast, wajumbe wa Jeshi la Ivory Coast, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Bw. Gbagbo, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Serikali ya Bw. Quattara, na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast kwa upande wa Bw. Quattara.

Katika raundi ya pili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ilimtangaza Bw. Quattara kuwa mshindi.
Lakini Baraza la Katiba ya nchi hiyo lilibadilisha matokeo kwa kutangaza Gbagbo kuwa mshindi baada ya kufuta matokeo ya kura katika majimbo saba ya wilaya 13 za eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiyo ngome ya Bw. Quattara.

Hatua hiyo ya Baraza la Katiba ilimpunguzia Bw. Quattara kura 600,000, sawa na asilimia 12 ya kura zote zilizopigwa.

4 comments:

  1. Hivi Jakaya anafikiria nini? Kwake hali ni mbaya Ivory Coast anafuata nini?

    ReplyDelete
  2. anatimiza ile kauli ya kujenga kwa mwenzio wakati kwako kunabomoka, aibu tupu kikwete na serikali yako ya kikomedy hv ndounaongoza nchi au unaigiza unahata haya kumetokea janga la mabomu tuna msiba unang'ng'na kwenda huko ilihali migogoro huku inakuandama why usimtume hata makamu wako ili tuamini unatupenda japo kidogo sjawahi kuona baba anawaachia msiba wanae afu yeye anakwenda kupatanisha familia za watu

    ReplyDelete
  3. Hawa wanaowateua wasuluhishi sidhani kama wana akili timamu. Naona wanaandaa kuweko na serikali ya pamoja, kitu ambacho ni cha ajabu na hakikubaliki. Uafrika tabu sana.

    ReplyDelete
  4. HAPO CHOKA MBAYA CHIZI ANAENDE KUMSULUHISHA CHIZI MWENZAKE .BUT IT IS SO PAINFULL TO SEE THIS HAPPENING IN AFRICA WHERE YOU CAN FIND THE COOLEST PEOPLE IN THE WORLD.LET PRAY FOR OUR CONTINENT AND FIGHT HARD TO BRING A PEACE WHERE OUR KIDS WILL SAY OUR MOTHER AND FATHER BROUGHT US TO PROMISSED LAND.BELEIVE ME WE CAN

    ReplyDelete